Umoja Wa Mataifa Wamtaka Kiongozi Wa Juu Wa Utawala Wa Kijeshi Myanmar Kujiuzulu

 

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Myanmar  siku ya Ijumaa  amemtaka kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo kujiuzulu na kurudisha madaraka aliyochukua kwa nguvu katika mapinduzi ya kijeshi Februari 1 kwa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia.

“Sioni utulivu wala mustakbali mwema wa Myanmar chini ya uongozi wa amiri jeshi huyu na Tatmadaw,” Christine Schraner Burgener ameiambia kamati ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za kibinadamu.

“Iwapo Jenerali wa Ngazi ya Juu Min Aung Hlaing anajali kikweli mustakbali wa nchi yake, ni lazima ajiuzulu na kukabidhi madaraka kwa serikali ya kiraia kulingana na matakwa ya wananchi,” amesema.

Tatmadaw ni jin la jeshi la Myanmar.

Schraner Burgener alitoa wito huo katika muhtasari wake wa mwisho alioutoa Umoja wa Mataifa. Ataachia madaraka ifikapo Oktoba 31, baada ya kushikilia madaraka hayo kwa miaka mitatu na nusu.

Ametumia muda wa miezi tisa akikabiliana na mapinduzi yaliyofanywa na jeshi, ambayo yamefanya Myanmar kuingia katika vurugu na uvunjifu wa amani. Zaidi ya raia 1,100 wameuawa, na maelfu kufungwa jela na zaidi ya watu 250,000 kupoteza makazi yao.

Rais Erdogan Wa Uturuki Aamuru Mabalozi 10 Wa Kigeni Kufukuzwa

 

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameamuru kufukuzwa kwa mabalozi wa nchi 10, zikiwemo Ujerumani na Marekani, walioomba kuachiliwa kwa kiongozi mmoja wa asasi za kijamii mzaliwa wa Paris, Osman Kavala. 

Mabalozi hao walitowa tamko la pamoja lisilo la kawaida siku ya Jumatatu wakisema kuendelea kushikiliwa mahabusu kwa mwanaharakati na mfadhili Kavala kunaijengea mashaka Uturuki.

"Nimemuamuru waziri wetu wa mambo ya kigeni kuwatangaza mabalozi hawa 10 kwamba ni watu wasiohitajika haraka iwezekanavyo," alisema Erdogan, akitumia istihali ya kidiplomasia inayomaanisha hatua ya kwanza kabla ya ufukuzwaji.

"Lazima waondoke hapa siku ile ile wasiyoijuwa tena Uturuki," aliongeza, akiwatuhumu mabalozi hao kwa "utovu wa adabu."

Siku ya Jumamosi (Oktoba 23), Erdogan alimuelezea Kavala kama "wakala" wa bilionea wa Kimarekani aliyezaliwa Hungary, George Soros, ambaye amekuwa akiandamwa mara kwa mara na wanasiasa wa mrengo wa kulia na wenye nadharia za hujuma dhidi ya Mayahudi. 

Habari Tano Za Soka Ulaya Jumapili October 24

 

Tetesi Za Soka Ulaya Jumapili October 24, 2021

1. Manchester United watafanya kila wawezalo ili kumbakiza kiungo mfaransa Paul Pogba Old Trafford huku Real Madrid ikiwa na matumaini ya kumsajili nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 mwishoni mwa msimu. 

2. Nahodha wa Wolves Conor Coady yuko kwenye orodha ya wanaowaniwa na klabu ya Newcastle United katika dirisha dogo la Januari huku ada ya mlinzi huyo wa England mwenye miaka 28 ikitajwa kuwa kama £20m. 

3. Mchezaji wa zamani wa Uholanzi Marc Overmars ameanza mazungumzo na Newcastle ili kuwa mkurugenzi wao mpya wa masuala ya soka. 

4. Chelsea imeonywa na Sevilla kwamba hawamuuzi kwa bei chee mlinzi wake wa kifaransa Jules Kounde, 22.

5. Mshambuliaji wa Atletico Madrid na Urguay Luis Suarez anataka kuendelea kusalia klabuni hapo hata baada ya msimu huu. Mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 34 amefunga mabao 5 msimu huu lakini mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu ujao. 

Benin Yaruhusu Utoaji Wa Mimba

 

Moja ya habari gumzo za wiki hii ni hii ya Wabunge wa Nchini Benin kupiga kura ya kuhalalisha utoaji mimba ambapo sasa Wanawake wa Nchi hiyo wanaweza kutoa mimba ndani ya miezi mitatu ya kwanza ya ujauzito kama wameona ujauzito huo unaweza kuwasababishia matatizo mbalimbali kwenye elimu, kazi, maadili au kama Mtoto huyo anaetarajiwa anaweza kuathiri maisha ya Mama.

Hata hivyo utoaji mimba kwenye Taifa hili la Afrika Magharibi ambako Wanawake karibu 200 hufariki kila mwaka wakati wakitoa mimba, ulikua ukiruhusiwa hapo kabla lakini kwa kesi maalum tu ambazo ni kama Mwanamke amebakwa, maisha ya mama yalikuwa hatarini kwasababu ya ujauzito au afya ya Mtoto aliyetarajiwa kuzaliwa itaathirika.

Sheria mpya ambayo imepitishwa wiki hii na kuligawa Taifa hilo pande mbili huku wengine wakikubali na wengine kukataa bado itasubiri kupitishwa kikatiba Mahakamani kabla ya kuanza kutekelezwa, pamoja na hayo imeungwa mkono na Viongozi mbalimbali wa Nchi hiyo akiwemo Waziri wa afya aliyesema italeta unafuu kwa Wanawake wengi ambao wanapata ujauzito wasioutaka.

Mambo Na Vitu Vidogo Vinavyoweza Kunogesha Penzi, Kulifanya Kuwa Lipya

Kila mmoja anapaswa kuwa furaha ya mwenzake. Anapaswa kumtendea mambo mazuri ili aweze kuwa na furaha na amani muda wote. 

Mwanaume anapaswa kushughulikia amani na furaha ya mwanamke wake, vivyo hivyo mwanamke ashughulikie furaha na amani ya mwanaume wake. 

Kuna vitu ambavyo mara nyingi huwa tunaviona ni vidogo lakini kimsingi huwa vina maana kubwa sana katika suala zima la uhusiano wa kimapenzi kwa mchumba au hata hatua ya ndoa.

MITOKO
Mara nyingi wapendanao huwa wanajisahau sana katika suala zima la mitoko ya hapa na pale. Mara nyingi kila mtu anajua kutoka kivyake na marafiki zake.

Mwanaume anatoka kwenda hoteli au sehemu mbalimbali za burudani na rafiki zake na mwanamke naye anatoka na mashoga zake. 

Ndugu zangu, hata kama kweli kila mtu ana mitoko yake lakini ni vyema kujiwekea utaratibu siku moja moja wapendanao mkatoka pamoja, ina maana kubwa sana.

ZAWADI
Lingine ni la vizawadi. Hata kama unajua kwamba mwenzako ana uwezo wa kununua kile ambacho wewe utamnunulia lakini fanya hivyo kama ishara ya upendo, inaleta maana kubwa sana katika uhusiano.

MPE KIPAUMBELE
Unapokuwa unawaza juu ya jambo fulani, mpe kipaumbele mwenzi wako kwa kuomba hata ushauri badala ya kuomba ushauri kwa marafiki zako, wafanyabiashara au wafanyakazi wenzako. 

Mwenzi wako anapoona humpi kipaumbele hususani katika masuala ya msingi, anaweza kuona ni kama unamdharau na hivyo kupunguza hamu ya kuwa na wewe.

MSAIDIE

Kuna wakati mwenzi wako anaweza kuwa anaweza kufanya jambo fulani lakini anapokuwa na wewe, anatamani wewe umsaidie, hilo nalo lina maana kubwa lifanye kadiri uwezavyo.

MJALI
Hili ni la muhimu sana, unaweza kuona kama halina maana sana lakini unapokuwa unamkumbusha mwenzi wako kuhusu suala la kula au kumuamsha asubuhi awahi kazini na mambo mengine kama hayo, yanaleta chachu na hamasa kubwa katika uhusiano.

Hali Ya Usalama Yaendelea Kuwa Tete Ethiopia

 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric Alhamisi wakati akizungumza na wanahabari mjini New York amesema kwamba hali ya kiusalama kaskazini mwa Ethiopia ni hatari na isiyotabirika.

ameongeza kusema kutokana na hali ilivyo katika wiki za karibuni, kwamba watoa misaada wanahofia kuongezeka kwa ghasia. 

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Dujarric amekumbusha pande zinazohusika kwenye mzozo huo kwamba ni lazima zizingatie sheria ya kimataifa za kibinadamu ili kulinda wakazi pamoja na miundombimu.

Amesema kwamba hali imedorora zaidi kutokana kuzuiliwa kwa upelekaji wa misaada kwenye jimbo la Tigray kupitia njia pekee iliyopo inayotokea Afar. 

Ripoti zinasema kwamba kati ya Oktoba 13 na 19, Umoja wa mataifa uliweza kufikisha malori 215 ya misaada kwenye jimbo la Tigray, ukiwa msaada zaidi kulinganisha na wiki iliyotangulia.

Dujarric ameongeza kusema kwamba tangu tarehe 12 Julai, malori 1,111 ya misaada yameingia Tigray ikiwa ni asilimia 15 pekee ya malori ya misaada yanayo hitajika jimboni humo. 

Amesema kwamba ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa jimbo hilo, malori 100 yanahitajika kuingia kila siku.

Ripoti zinaongeza kwamba malori ya mafuta bado yamezuiliwa kuingia Tigray, wakati 14 yakisemekana kukwama kwenye mji wa Semera jimboni Afar.

Jinsi Ya Kusafisha Kinywa Chako Kwa Kutumia Mswaki, Hatua 6 Muhimu

Piga mswaki angalau mara mbili kwa siku baada ya chai na baada ya chakula cha usiku.

Tumia dawa ya meno yenye madini ya fluoride.
Badili mswaki kila baada ya miezi mitatu
Muone daktari wa meno mara kwa mara kwa uchunguzi na matibabu ya mapema.

HATUA ZA KUPIGA MSWAKI.
1. Weka mswaki wako katika degree 45 na meno yako ili mswaki wako ugusane na meno yako pamoja na fizi.

2. Sugua sehemu ya nje ya meno yako Dk 2-3 taratibu bila kutumia nguvu kwa mwendo wa kuzungusha kisha sogea kwenye meno mengine Dk 2-3 na rudia hivyo hivyo.

3. Endelea vile vile kwa meno ya ndani, mswaki ukiwa kwenye degree 45 na meno yako kwa mwendo wa kuzungusha mbele na nyuma kwenye meno na fizi zote.

4. Geuza mswaki wako nyuma ya meno ya mbele kisha kwa mwendo wa kwenda juu na chini safisha meno hayo vizuri.

5. Weka mswaki wako kwenye sehemu ya meno ya kutafunia na kwa taratibu safisha sehemu hizo kwa mwendo wa kwenda nyuma na mbele.

6. Malizia kwa kusafisha ulimi vizuri ukielekea kama kooni(Kuwa makini unapofanya hivyo usije ukafikisha mswaki kooni ukatapika)

Dokezo Za Usafi Kabla Na Baada Ya Tendo La Ndoa (Kujamiiana)

 

Kidokezo kimoja ambacho kinastahili kuzingatiwa na jinsia zote mbili kwa mujibu wa wataalamu ni kwamba wanaume na wanawake wanashauriwa kwenda haja ndogo kabla na baada ya kufanya tendo la ndoa.

"Kwenda haja ndogo baada ya kufanya tendo la ndoa ni moja ya njia muhimu ya kujiepusha na magonjwa yanayosababishwa na bakteria, " anasema Martínez.

"Kujisaidia haja ndogo baada ya tendo la ndoa kunasaidia kusafisha kibofu cha mkojo, hali ambayo inazuia bakteria kuathiri sehemu hiyo," anaeleza

"Pia kwenda haja ndogo kabla ya tendo la ndoa ni muhimu, kwani wapenzi watakaribiana bila kuwa na hofu ."

Briet anaongeza kuwa mwenendo huo "ni mzuri kwani unaweza kuzuia magonjwa yanayoathiri njia ya kupitisha mkojo kwa kiwango kikubwa hata kama sio magonjwa mengine."

Wataalamu wa saikolojia ya ngono wanapendekeza wapenzi kwenda haja ndogo "punde baada ya kufanya tendo la ndoa" ili kujikinga na magonjwa na kupunguza uwezekano wa kuambukizwa magonjwa.

Kulingana na wataalamu hao wanawake wako katika hatari ya kupata maabukizi ya magonjwa yanayoathiri njia ya kupitisha mkojo. Hivyo basi wanapendekeza wawe na mazoea ya kwenda haja dakika 15 kabla ya kushiriki tendo la ndoa.

Utafiti uliochapishwa katika jarida la matibabu la ustawi wa familia(2002) unasema kuwa wanawake wenye afya ambao huenda haja dakika 15 kabla ya kujamiiana huenda wakajiepusha na hatari ya kupata maambukizi wakilinganishwa na wenzao ambao hawafanyi hivyo.

Mapendekezo makuu:

Osha sehemu za siri kila siku kwa kutumia maji.

Piga mswaki.

Valia nguo za ndani safi, zilizotengenezwa kutokana na pamba ni bora zaidi.

Muone daktari angalau mara moja kwa mwaka ufanyiwe uchunguzi wa kimatibabu.

Kuwa na mazoea ya kujichunguza endapo utaona mabadiliko yoyote katika sehemu za siri muone dakatari.

Tumia kondomu wakati wa tendo la ndoa.

Inapendekezwa usiwe na mazoea ya kunyoa nywele zote zinaoota katika sehemu za siri, kwasababu zinatumika kama kinga, bora kupunguza kidogo.

Virusi Vya Covid Huenda Viliwaua Wahudumu Wa Afya Kati Ya Elfu 80 Hadi 180-WHO

 

Virusi vya Covid 19 vimeathiri vibaya wafanyikazi wa huduma ya afya na huenda viluwaua kati ya 80,000 na 180,000, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linasema.

Wafanyakazi wa huduma ya afya lazima wapewe kipaumbele kwa chanjo, mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema

Vifo hivyo vilitokea kati ya Januari 2020 na Mei mwaka huu.

Hapo awali, afisa mwingine mwandamizi wa WHO alionya ukosefu wa chanjo unaweza kuona janga hilo likiendelea hadi mwaka ujao.

Kuna takriban wafanyakazi milioni 135 wa huduma za afya ulimwenguni.

"Takwimu kutoka nchi 119 zinaonyesha kuwa kwa wastani, wafanyikazi wawili kati ya watano wa huduma za afya ulimwenguni wamepewa chanjo kamili," Dk Tedros alisema.

Raisi Wa Marekani Aaahidi Kuilinda Taiwani Dhidi Ya Mashambulizi Ya China

 

Rais wa Marekani Joe Biden amesema nchi yake itatetea Taiwan ikiwa Uchina itashambulia, hatua ambayo inatofautiana hadharani na sera ya muda muda mrefu ya Marekani

"Ndio, tuna wajibu wa kufanya hivyo," alisema alipoulizwa katika ukumbi wa mji alipoulizwa iwapo Marekani itailinda Taiwan .

Lakini msemaji wa Ikulu baadaye aliambia baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani kwamba matamshi yake hayakuashiria mabadiliko ya sera.

Marekani kwa muda mrefu imekuwa ikifanya "utata wa kimkakati" linapokuja suala mwiba wa kutetea Taiwan.

Hii inamaanisha kuwa Marekani imekuwa na msimamo wenye utata kwa makusudi juu ya kile itakachofanya ikiwa China itashambulia kisiwa hicho.

Marekani haina uhusiano wowote wa kidiplomasia na Taiwan, lakini inauza silaha kwa kisiwa hicho kama sehemu ya Sheria ya Uhusiano ya Taiwan, ambayo inasema kuwa Amerika lazima isaidie Taiwan kujilinda .

China inaona Taiwan kama jimbo lililojitenga, ambalo linaweza kuchukuliwa tena kwa nguvu siku moja ikiwa ni lazima, wakati Taiwan inadai kuwa ni nchi huru.

Mvutano umekuwa ukiongezeka kati ya nchi hizo mbili katika wiki za hivi karibuni baada ya Beijing kurusha ndege kadhaa za kivita katika eneo la ulinzi wa anga la Taiwan.

Utawala wa Rais Joe Biden uliidhinisha mauzo mengine ya kibiashara ya moja kwa moja kwa Taiwan tangu achukue madaraka mapema 2021, na imetaka kuimarisha uhusiano zaidi na kisiwa hicho, na kusababisha hasira kutoka Beijing.

Ijue Maana Ya Hangover Na Kukabiliana Nayo

Kuna pombe au vilevi vya aina tofauti kama vile bia, wine, pombe kali. Watu wengi hupenda kujiburudisha kwa kunywa vinywaji hivi na kati yao kuna ambao wanajikuta baada ya kunywa kwa kupitiliza wamepata hali ya kutapika, kichwa kuuma, kizunguzungu, usingizi mkali, uchovu wa mwili n.k, hali ambayo ni maarufu kama “Hangover”.

Hali hii inaweza kuanza masaa machache baada ya kuacha kunywa kilevi hadi masaa 24. Kikubwa kinachosababisha hali hii ni kuwa na kiasi kikubwa kupitiliza cha kilevi mwilini. 

Hii inatokana na kwamba kiasi cha kilevi kinacho tolewa mwilini hakibaliki kadiri ya kiasi cha kilevi ambacho mtu atatumia (Zero order kinetics).

Inamaana kama litre 1 moja ya kilevi inatolewa ndani ya saa moja, kwahivyo endapo mtu atakunywa litre 5 za kilevi ndani ya saa moja bado kiasi ambacho kitatolewa mwilini kitabaki kuwa litre moja ndani ya saa moja. 

Hali hii inasababisha ulimbikaji wa pombe mwilini. Ulimbikaji huu huongeza kasi katika athari za pombe mwilini. Hali ambayo inafahamika kama “hangover”

Uwezo wa mwili kukabiliana na kiasi cha kilevi ambacho mtu amekunywa inatofautiana kati ya mtu hadi mtu kulingana na:

Kiasi cha pombe ambacho mtu anakunywa mara kwa mara.  Endapo mtu hunywa pombe mara kwa mara, uwezo wa mwili wake kukabiliana na pombe huongezeka.
Vinasaba vya mtu ambavyo vinaamua kiasi na aina za protini za umeng’enyuaji zinazotengenezwa.
Magonjwa ambayo yaweza sababisha kupungua au kuongezeka kwa kiasi cha uondoaji wa pombe.
Utumiaji wa pombe na dawa ambazo zinaathiri mlorongo wa  umeng’enyuaji wa pombe.

Je, ninawezaje kuondoa hali ya “Hangover”?
Hali hii ya hangover huisha pale ambapo mwili umeweza kutoa pombe kufikia kiasi kidogo hivyo mwili unahitaji muda kuendelea kuondoa pombe ili uweze kurejea hali ya kawaida. Katika muda huu unaweza kufanya yafuatayo ili kuusaidia mwili kuondoa pombe hii:

1. Kunywa maji ya kutosha.
2. Kula chakula chenye vitamin B complex vinavyohitajika katoka umeng’enyuaji wa pombe kama vile nyama aina nyingi( ng’ombe, mbuzi, kuku, samaki), mayai, maziwa, viazi, maharagwe n.k
3. Kula /kunywa vitu vyenye sukari

Habari Tano Kubwa Za Soka Ulaya Ijumaa October 22

 

Tetesi Za Soka Ulaya Ijumaa October 22, 2021

1. Barcelona inataka kuishinda Real Madrid katika mbio za kumsajili mshambuliaji wa PSG na Ufaransa Kylian Mbappe, ambaye mkataba wake unamalizika msimu unaokuja. 

2. Real Madrid watamkosa mshambuliaji wa Borussia Dortmund Erling Braut Haaland,21, huku Manchester City, Paris St-Germain au Bayern Munich kuna uwezekano mkubwa akatua huko. 

3. Borussia Dortmund wamekasirishwa na kitendo cha kocha wa Chelsea Thomas Tuchel kuzungumza hadharani kuhusu nia ya klabu yake ya kumsajili Haaland. 

4. Everton wanamtaka kiungo wa Manchester United na England Jesse Lingard, 28, mwezi Januari. 

5. Kocha wa United Ole Gunnar Solskjaer anasema klabu hiyo haijapokea ofa kutoka Everton kwa ajili ya kiungo wake wa Uholanzi Van de Beek, licha ya uwepo wa tetesi nyingi. 

Trump Kuja Na Mtandao Wake Wa Kijamii Ambao Utakuwa Mshindani Wa Facebook Na Twitter

 

Rais Mstaafu wa Marekani, Donald Trump anakusudia kuzindua mtandao wake wa kijamii, Truth Social, ambao anasema utakuwa mshindani wa mitandao mikubwa kama Twitter & Facebook.

Mitandao mbalimbali ilimfungia Trump baada ya mamia ya wafuasi wake kuvamia Bunge la Marekani Januari 6.

Alexei Navalny Atunukiwa Tuzo Ya Bunge La Ulaya Sakharov

 

Kiongozi wa upinzani nchini Urusi aliye gerezani ambaye pia ni mkosoaji mkubwa wa rais Vladmir Putin, Alexei Navalny ametunukiwa tuzo ya juu kabisa inayotolewa na Umoja wa Ulaya kuhusu haki za binadamu. 

Katika ishara ya wazi ya ukosoaji kwa Ikulu ya Kremlin, viongozi wa bunge la Umoja wa Ulaya wamemteua Navalny kupokea tuzo hiyo kutoka kundi lililojumuisha wagombea wengine ikiwemo rais wa zamani mpito nchini Bolivia Jeanine Anez. 

Tangazo kuhusu tuzo hiyo limetolewa kupitia ukurasa wa Twitter wa Bunge la Ulaya likiwa pia na ujumbe wa kuzitaka mamlaka nchini Urusi kumuachia huru kiongozi huyo wa upinzani aliyekamatwa na kutupwa gerezani mwazoni mwa mwaka huu. 

Uamuzi wa kumtunuku tuzo hiyo Navalny yumkini utadhoofisha zaidi mahusiano yaliyopwaya kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi tangu Moscow ilipoinyakua kwa nguvu rasi ya Crimea mwaka 2014 na ilipotuhumiwa kuhusika na shambulizi la sumu dhidi ya Navalny.

Mzozo Kuhusu Chanjo Za Covid-19 Waongezeka Marekani

 

Mzozo kuhusiana na utoaji wa chanjo za corona Marekani, huenda ukaongezeka katika wiki zijazo wakati amri mpya inayohitaji watu kuchukua kwa lazima ikikaribia kuanza kufanya kazi. 

Maafisa wa ikulu ya Marekani wanaendelea kukarabati amri ya rais Joe Biden, kwamba takriban wafanyakazi milioni 80 kwenye sekta ya biashara wapatiwe chanjo ili kuendelea kufanya kazi au wawe wakipimwa mara kwa mara iwapo wapo kwenye makampuni yenye zaidi ya wafanyakazi 100.

Hatua hiyo inawahitaji wafanyakazi wote wa serikali pamoja na wanajeshi kupokea chanjo hiyo kabla ya mwaka kumalizika. Ingawa wengi wa wanajeshi wa majini wa Marekani tayari wamepokea chanjo, baadhi ya maafisa wameanza kuwafukuza wale waliokataa.

Wakati huo huo, baadhi ya makampuni makubwa pamoja na mashirika yameanza kuwafukuza kazi wale waliokataa kupokea chanjo licha ya kwamba tayari wamarekani milioni 177 wamepokea chanjo hiyo ikiwemo thuluthi mbili ya watu wazima hapa nchini.

Baadhi ya wanajeshi wameanza kuweka video zao kwenye mitandao wakieleza masaibu wanayopitia kutokana na kukataa kupokea chanjo hiyo. Baadhi wanadai kwamba haki zao za kimsingi za kufanya maamuzi ya kiafya zinahujumiwa.

Polisi Wazima Maandamano Eswatini

 

Mkuu wa chama cha wafanyakazi cha Eswatini Oscar Nkambule amesema kwamba takriban watu 80 wamejeruhiwa Jumatano wakati wa maandamano ya kuitisha demokrasia yanayoendelea nchini humo.

Chama hicho cha wafanyakazi kwa jina NAPSAWU kimesema kwamba wanachama wake 50 walipelekwa hospitalini kwenye mji mkuu wa Mbabane huku wengine 30 wakipelekwa kwenye mji wa Manzini.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, mamia ya wanajeshi na polisi wanasemekana kufanya misako kwenye miji hiyo miwili wakati wakirusha gesi ya kutoa machozi pamoja na risasi za mipira kwa vikundi vya watu vilivyo kusanyika. Serikali pia inasemekana kufunga huduma za internet baada ya picha na video za ghasia kuanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Nkambule ameambia AFP kwamba ghasia zilianza saa moja ya asubuhi wakati akilaumu maafisa wa usalama kwa kurusha gesi ya kutoa machozi kwenye basi lililobeba wafanyakazi waliokuwa wakiandamana. Baadhi ya video zilizosambazwa zinaonyesha baadhi ya watu wakiruka kutoka kwenye madirisha ya basi hilo likiwa limezingirwa na moshi mweupe.

Kenya Yaondoa Marufuku Ya Kutembea Usiku

 

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza kuondolewa kwa marufuku ya nchi nzima ya kutembea usiku iliyowekwa tangu mwezi Machi mwaka 2020 kama sehemu ya juhudi za kupambana na janga la virusi vya corona. 

Akihutubia taifa katika kilele cha siku ya Mashujaa mjini Nairobi, rais Kenyatta amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kupungua kwa kisia kikubwa kiwango cha maambukizi ya Covid-19 kwenye taifa hilo la Afrika Mashariki. 

Licha ya hatua hiyo, rais Kenyatta amewarai wakenya kuendelea kuheshimu kanuni zote za kiafya ili kufanikisha kurejea kwa maisha ya kawaida nchini humo. 

Kenya, taifa la watu milioni 54 limerikodi visa 252,000 vya maambukizi ya virusi vya corona na vifo vya zaidi ya watu 5,000 tangu kuzuka kwa janga hilo na hivi sasa linaendelea na kampeni kubwa ya utoaji chanjo dhidi ya maradhi hayo.