KUWASHWA katika
ngozi ya mwili ni kitu kinachomfanya mwanadamu kukosa utulivu kutokana na kero
anayopata. Hutokea mwanadamu kukumbwa na muwasho wa hata kuaibisha ikiwamo ule
wa sehemu za siri.
Lakini wataalamu
wanasema tatizo la kuwashwa linaweza kumwathiri mtu kiasi cha kumsababishia
matatizo ya kiakili ikiwamo kujitenga, kutojiamini mbele za watu, kuwa na aibu,
huzuni na sonona.
Tatizo la kuwashwa
mwili linaweza kuwa ni la muda mfupi tu na likaisha, lakini inapotokea tatizo
likawa la mara kwa mara kwa zaidi ya siku 14, maana yake limekuwa sugu.
Kuwashwa pia kunaweza kuambatana na hali ya kupata viuvimbe, vimiinuko kama
mawimbi au vipele katika ngozi kutegemeana na chanzo.
Na wakati mwingine
muathirika hujikuta hata rangi ya mahali panapomuwasha, huweza kubadilika rangi
na kuwa pekundu. Kuwasha ngozi ya mwili inaweza kuwa ni dalili ya uwepo wa
maradhi yanayoleta mapele au kubabuka ngozi na vilevile inaweza kuwa ni dalili
ya kuwepo kwa maradhi ya figo na ini.
Viko vitu
mbalimbali ambavyo mara kwa mara huchangia kujitokeza kwa hali ya muwasho
ambayo huweza kuwa na asili ya kemikali, vimelea, vumbi, vyakula na dawa.
Nikianza na tatizo la ukavu wa ngozi ambalo kitabibu linaitwa ‘Xerosis’. Hili
husababishwa na matokeo ya vitu vilivyomo katika mazingira yakiwamo ya hali ya
hewa ya joto au ya baridi.
Mfano mtu akitumia
kiyoyozi kwa muda mrefu au kuoga maji, kunaweza kuleta ukavu katika ngozi na
kusababisha muwasho. Sababu ya pili ni maradhi ya ngozi na yale yanayoleta
mapele ikiwamo ukurutu, vipele vya tete maji, shambulizi la ngozi na mba au
fangasi.
Mengine ni maradhi
ya ogani za ndani ya mwili kama zikishindwa kufanya kazi, husababisha mwasho.
Ogani hizo ni pamoja na ini na figo. Kama zikishindwa kufanya kazi, zinaweza
kusababisha mrundikano wa taka sumu zinazoweza kusababisha mwili kuwasha.
Vilevile maradhi
ya saratani, maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na maradhi ya tezi ya
shingo, pia yanaweza kuleta muwasho. Pia, kuathirika kwa mishipa ya fahamu,
inaweza kusababisha mtu kupata hali ya muwasho, mfano wagonjwa wa kisukari na
mkanda wa jeshi, huharibu mishipa ya fahamu na kuwafanya wapate hisia za
kuwasha.
Vitu kama nguo,
kemikali, sabuni tunazoogea, mafuta, krimu, vipodozi na vumbi, pia vinaweza
kuleta uchokozi na kusababisha kutokea kwa mzio (allergy).
Mzio hutokea baada
ya mwili kuchokozwa na kujibu mapigo na kutiririsha kemikali za mfumo wa kinga
zinazosababisha kuwasha. Vilevile mtu anaweza kupata mzio baada ya kula
vyakula, mfano vyakula vinavyoongoza kuleta hali kama hizi ni pamoja na mazao
ya baharini na jamii ya karanga.
Baadhi ya dawa za
antibayotiki, fangasi, malaria na za maumivu zinaweza kuwa na madhara madogo
ikiwamo ya kumsababishia mtu mwasho na vipele. Hali ya kuwa ujauzito huleta
mabadiliko ya kimwili yanayoweza kuchangia wajawazito kupata muwasho hasa
katika maeneo ya tumboni, mikononi, mapajani na katika matiti.
Ikumbukwe unaweza
ukapata muwasho na kutumia kasi na nguvu kujikuna mpaka kusababisha michubuko
katika ngozi ambayo inaweza kuleta majeraha na kukaribisha uvamizi wa vimelea
mwilini. Hivyo, ni vizuri kuepuka kujikuna na badala yake tumia matibabu salama
ya nyumbani ambayo huandaliwa na vitu ambavyo tunavyo katika sehemu tunazoishi.
TIBA
Maji safi na
salama ya bombani ni moja ya tiba salama ya mwasho, unaweza kutumia maji
yanayotiririka na kuyalengesha katika eneo lenye mwasho.
Au tumia bomba la
mvua la kuogea kujimwagia mwilini kama mwasho uko sehemu kubwa ya mwili.
Vilevile unaweza kutumia kitambaa au taulo safi na kulichovya katika maji kisha
weka panapowasha.
Maji yanasaidia
kuondoa vitu vilivyoshikamana na ngozi vinavyosababisha kuwasha, vilevile maji
hupoza muwasho katika ngozi na kufifisha kukereketa.
EmoticonEmoticon