#ENEWS:Nicki Minaj Avunja Tamasha Lake Saudi Arabia

Mwanamuziki Nicki Minaj amelazimika kuvunja tamasha alotakiwa kulifanya nchini Saudi Arabia wiki ijayo akisema anaunga mkono haki za wanawake na wapenzi wa jinsia moja.
Taarifa za nyota huyo wa miondoko ya rap kutumbuiza Saudia ziliwashtua wengi na kusababisha kelele kali kutoka kwa wanaharakati wanaokosoa rekodi ya haki za binadamu ya nchi hiyo.
Wengine wakawa wanajiuliza msanii huyo atavaaje kwenye tamasha hilo kwa kuwa nchi hiyo inafuata mfumo wa kihafidhina wa Kiislamu, na Minaj ni maarufu kwa kuvaa nusu uchi.
Saudi Arabia imekuwa ikijaribu kulegeza vikwazo kwenye sekta ya burudani ili kukuza sekta ya sanaa kwa ujumla ya nchi hiyo.
"Japo ninapenda kwelikweli kutumbuiza mbele ya mashabiki zangu nchini Saudia, lakini baada ya kujipatia elimu zaidi kwa masuala kadhaa, naamini ni muhimu kwangu kuweka wazi kuwa naunga mkono haki za wanawake, wapenzi wa jinsia moja na uhuru wa kujieleza."
Ijumaa iliyopita, Taasisi ya Haki za Binaadamu yenye maskani yake nchini Marekani ilimuandikia barua ya wazi Minaj ikimtaka aachane na taasha hilo la Julai 18.
Walimuomba nyota huyo "akatae pesa za utawala (wa nchi hiyo)" na kutumia ushawishi wake kushinikiza kuachiliwa huru kwa wanaharakati wanawake waliokamatwa.


EmoticonEmoticon