Kauli Ya Msanii/Mbunge Jaguar Wa Kenya Baada Ya Kufika Tanzania

Mbunge wa Starehe nchini Kenya, Charles Njagua maarufu Jaguar yupo nchini Tanzania kuanzia jana Ijumaa Julai 18, 2019.
Huku akieleza kuwa atakuwa Tanzania hadi Jumapili Julai 21, 2019, Jaguar amesema hana tatizo na Watanzania.
Juni 25, 2019 mbunge huyo ambaye pia ni mwanamuziki kupitia mitandao ya kijamii video yake ilisambaa akieleza kuwafukuza wafanyabiashara wa kigeni wakiwemo Watanzania ndani ya masaa 24 kurudi kwao la sivyo watawapiga na kuwarudisha nchini mwao.
Serikali ya Kenya ililaani kauli yake hiyo na kusema si msimamo wa nchi hiyo, pia alikamatwa na kusota rumande kwa siku nne katika kituo cha Polisi Kileleshwa baada ya mahakama kusema kuna haja ya kulinda uchunguzi unaoendeshwa kuhusu matamshi ya uchochezi anayodaiwa kuyatoa. Hata hivyo aliachiwa kwa dhamana.
Akizungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) jana Julai 18, 2019, Jaguar amesema amekuja Tanzania kwa kuwa hana tatizo na Watanzania na kauli aliyoitoa hakuwa amewalenga wao, bali wanaofanya biashara kinyume na taratibu za Kenya.
Nimekuja kutembea Tanzania naipenda Tanzania na kama unavyojua ile kauli ambayo watu walishindwa kuielewa, nilikuwa namaanisha wanaofanya kazi kinyume na taratibu,” amesisitiza.
Alipoulizwa kuhusu kuomba msamaha kwa kauli hiyo, amesema hana cha kusema na hajakosea, akisisitiza kuwa aliwalenga wanaofanya biashara kinyume na taratibu.
Alipoulizwa kilichomleta Tanzania, amesema familia yake ipo Tanzania amekuja kuiona.
Pia nina marafiki kama Joseph Haule (Profesa J- mbunge wa Mikumi)   pamoja na Joseph Mbilinyi (Sugu-mbunge wa Mbeya Mjini). Hawa nitapata nafasi ya kukutana nao,” amesisitiza.


EmoticonEmoticon