Messi Na Wenzake Watakiwa Kurudisha Magari Waliyopewa Na Kampuni....

Kampuni ya magari ya Audi imewataka mastaa wa Barcelona wakiongozwa na Lionel Messi kurudisha magari waliyopewa na kampuni hiyo baada ya mkataba wa udhamini kati ya kampuni hiyo na Barcelona kukoma.
Messi pamoja na mastaa wengine wa Barcelona walipewa fursa ya kuchagua magari ya kifahari ya AUDI wanayoyataka baada ya kampuni hiyo kutoka Ujerumani kuingia katika ushirikiano wa kibiashara na Barcelona mwaka jana.
Messi alichagua gari aina ya Audi RS 6 Avant yenye thamani ya Pauni 130,000 wakati kiungo wa kimataifa wa Croatia, Ivan Rakitic ambaye hatima yake bado ipo shakani Nou Camp aliamua kuchagua gari aina ya Audi Q7 yenye thamani ya pauni 65,000.
Lakini, sasa kampuni hiyo imeyataka magari hayo katika yadi yake baada ya kumaliza mkataba na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Hispania tangu Juni 30, mwaka huu na imewapa wiki tatu tu mastaa hao kurudisha magari hayo ya kifahari.
Wachezaji hao wamekuwa wakiyatumia magari hayo kwa safari za kila siku kwenda na kurudi katika uwanja wa mazoezi Ciutat Esportiva Joan Gamper uliopo kando ya Jiji la Barcelona, ingawa baadhi wamekuwa wakitumia magari binafsi.
“Mwaka jana, mmoja kati ya mabosi wa kampuni hiyo ya Audi, Christian Guenthner alikaririwa akisema “Kwa shughuli maalum za kibiashara wanatumia magari ya Audi. Wakati wa kuchagua magari hayo kampuni na klabu zilishirikiana kwa karibu zaidi.


EmoticonEmoticon