#SPORTS:Lampard Aahidi Hili Na Kuwaambia Wachezaji Wake...

Kocha mpya wa Chelsea, Frank Lampard amewaambia wachezaji wake tena kwa msisitizo kwamba ni lazima wamalize ndani ya Top Four kwenye Ligi Kuu England msimu ujao.

Wababe hao wa Stamford Bridge kwa sasa wanakabiliwa na adhabu ya kufungiwa kusajili kwa kipindi cha miaka miwili, lakini wamefanikiwa kumbakiza kiungo Mateo Kovacic kwenye kikosi chao baada ya kumbeba jumla kutoka Real Madrid kufuatia mkataba wake wa mkopo kufika mwisho.
Chelsea waliwalipa Madrid Pauni 40 milioni ili kunasa huduma ya Kovacic moja kwa moja, aendelee kuwapo kwenye kikosi chao kwa ajili ya mapambano ya kwenye Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kwenye dirisha la usajili wa Januari, Chelsea walinasa huduma ya Christian Pulisic kutoka Borussia Dortmund kwa ada ya Pauni 58 milioni na kisha kumbakiza kwa mkopo kwenye klabu hiyo ya Ujerumani, lakini sasa atajiunga na wababe hao wa Stamford Bridge katika dirisha hili.
Lampard alisema: "Nimecheza hapa kwa miaka mingi, nafahamu vigezo. Tunahitaji kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya kila mwaka. Hilo ndilo jambo tunalopaswa kulifanya.
"Ni jambo la wazi kabisa, limejionyesha bayana kwa miaka ya karibuni kwamba tumekuwa na kikosi bora kinachotufanya tuwepo kwenye Top Four."


EmoticonEmoticon