#SPORTS:Nyota Wanaosaka Uhamisho Kwa Nguvu

Romelu Lukaku
Alipoulizwa na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita juu ya mustakabali wake katika kikosi cha Man United, Lukaku akajibu: "subirini wiki ijayo mtajua kitu."
Lukaku amekuwa akihusishwa na kuhamia katika klabu ya Inter Milan, na imefahamika kuwa uhamisho wake utategemea na kitakachotokea kwa Icardi.
Hivyo endapo Icardi atauzwa wiki hii, ni dhahiri kuwa uhamisho wa Lukaku kujiunga na klabu hiyo utakuwa umeiva.
Lukaku ameambatana na kikosi cha United kwa sasa kilichopo kwenye ziara ya maandalizi ya msimu mpya nchii Australia na Singapore.
Mshambuliaji huyo hakuwa na wakati mzuri msimu uliopita na amekuwa akishutumiwa kwa kushuka kiwango.

Paul Labile Pogba

Upande wa Pogba kumekuwa na sarakasi za kutosha na zilikolea pala mchezaji huyo aliposema mwezi uliopita kuwa ''sasa inaweza kuwa muda mzuri wa kuhamia sehemu nyingine''.
Ni dhahiri kuwa si kocha Ole Gunnar Solskjaer wala uongozi wa Man United unaotaka mchezaji huyo nyota kuondoka Old Trafford katika dirisha hili la usajili la majira ya joto.
Wiki iliyopita, wakala wa mchezaji huyo Raiola aliliambia gazeti la The times kuwa mchezaji wake anataka kuondoka, na klabu hiyo inajua fika nia ya mteja wake.
Vilabu vya Real Madrid na Juventus vinaripotiwa kutaka kumsajili kiungo huyo Mfaransa mwenye miaka 26 japo hakuna kati yao ambaye amepeleka maombi rasmi ya kutaka kumnunua.

Matthijs de ligt
De Ligt naye ni nahodha na hajaungana na timu yake kwenye kambi ya maandalizi na anasaka uhamisho kwa nguvu kama Koscienly.
Tofauti baina yao ni kuwa, De Ligt ana baraka zote kutoka uongozi wa Ajax juu ya kile afanyacho.
Ajax kwa sasa wapo kwenye kambi ya maandalizi nchini Austria na nahodha wao amebaki Amsterdam akisubiri kukamilika kwa uhamisho kwenda moja ya klabu kubwa Ulaya.
Beki huyo wa kati kisiki ni kinda kiumri, ana miaka 19 tu, lakini ameiongoza Ajax kuchukua ubingwa wa Uholanzi msimu uliopita na kufika fainali ya klabu bingwa Ulaya ambapo walifubgwa na Liverpool.
De Ligt anawindwa na Barcelona, Juventus, Manchester United na Paris St-Germain.
Wiki iliyopita, rais wa klabu ya Barcelona Josep Bartomeu alisema anajua wapi mchezaji huyo atacheza msimu ujao.
Machampioni wa Italia klabu ya Juventus wanatajwa kuwa ndio wanaoweza kuinasa saini ya beki huyo na wanatarajiwa kutoa kitita cha pauni milioni 71.
 
Laurent Koscielny
Huyu ni nahodha wa washika bunduki wa London klabu ya Arsenal.
Koscienly mwenye miaka 33 alijiunga na Arsenal mwaka 2010 na bado yungali na mkataba na klabu hiyo mpaka mwishoni mwa msimu wa 2019/2020.
Hata hivyo ameweka wazi nia yake ya kutaka kuondoka klabuni hapo katika dirisha hili la usajili.
Nahodha huyo ameenda mbali kwa kufikia hatua ya kugoma kusafiri na timu kwenye kwenye ziara ya kujiandaa na msimu mpya nchini Marekani.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Arsenal imeeleza kusikitishwa kwake na hatua hiyo ikisema ni "kinyume kabisa na maelekezo yetu kwa mchezaji."
Klabu tatu za nchini Ufaransa Bordeaux, Rennes na Lyon zimeonesha nia ya kutaka kumsajili mchezji huyo.
Inaarifiwa kuwa Bordeaux imempa ofa ya mkataba wa miaka mitatu.
Mchezaji nyota wa zamani wa Arsenal, Ian Wright amemtahadharisha Koscienly kuwa matendo yake ya sasa yatamfanya afute kumbukumbu zote nzuri alizojijengea kwenye mioyo ya mashabiki wa Arsenal kwa miaka 9.
Mauro icardi
Tofauti na De Ligt na Koscienly, Icardi alivuliwa unahodha wa klabu yake mwezi Februari mwaka huu.
Icardi naye hayupo kwenye kambi ya maandalizi ya Inter Milan na mshambuliaji huyo anatarajiwa kuuzwa kwenda klabu nyengine hivi karibuni.
Kama ilivyo kwa De Ligt Icardi amekubaliana na uongozi wa klabu hiyo kutokuwa sehemu ya kambi ya maandalizi.
Juventus ndiyo imekuwa ikitajwa zaidi katika mbio za kumsajili lakini mpaka saasa hakuna mazungumzo rasmi yaliyofanyika.
Napoli pia wanahusishwa na kumtaka sawia na AS Roma japo itakuwa vigumu kwa Icardi kwenda Roma ambao hawatashiriki Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.


EmoticonEmoticon