#SPORTS:Senegal Yatinga Fainali AFCON 2019

Goli la kujifunga la Tunisia katika muda wa nyongeza limewavusha Sengal mpaka hatua ya fainali ya kombe la Mataifa ya Africa (AFCON) kwa mwaka 2019.
Japo wengi waliipigia chapuo Senegal kushinda mchezo huo, lakini ushindi haukuwa rahisi, na Tunisia 'wamekufa wakipambana'.
Dakika 90 zilitamatika bila timu yoyote kupata ushindi, huku pande zote mbili zikikosa penati katika kipindi cha pili.
Ushindi ulipatikana kwa Senegal ndani ya dakika 30 za nyongeza.
Kipa wa Tunisia Moez Hassen alifanya makosa katika dakika ya 100 kwa kuokoa vibaya mpira wa krosi na kumgonga beki wake Dylan Bronn na kuzama wavuni.
Katika dakika za mwisho za mchezo huo kukatokea 'tafrani' baada ya refa kutoa penati golini mwa Senegal kwa madai kuwa kiungo Idrissa Gana Guaye ameunawa mpira.
Hata hivyo penati hiyo ilikataliwa baada ya refa kwenda kujihakikishia kwenye mwamuzi wa msaada wa televisheni (VAR).
Hii ni mara ya pili kwa Senegal kutinga hatua ya fainali. Mara ya kwanza ikiwa 2002 ambapo walipoteza kwa mikwaju ya penati dhidi ya Cameroon.
Safari ya Tunisia kutaka kulichukua kombe hilo kwa mara ya pili imetamatika mpaka hapo yatakapofanyika mashindano mengine.


EmoticonEmoticon