Arsenal Wagonga Mwamba Kumpata Beki Wa Juventus

Jaribio la Arsenal kumpata kwa mkopo beki wa Juventus, Daniele Rugani, limegonga mwamba baada ya mabingwa hao wa Italia kuwatolea nje
.
Arsenal wanafukuzia kuimarisha safu yao ya ulinzi ambayo msimu uliopita ilikuwa inavuja kama chujio ikiruhusu magoli 50 na nafasi ya beki wa kati na wa kushoto ndizo zinazowaumiza kichwa.

Beki wa kushoto wa Celtic, Kieran Tierney, 22, anaendelea kuwa chaguo lao la kwanza katika nafasi hiyo, huku ofa zao mbili za kwanza zikikataliwa na klabu hiyo ya Scotland.

Lakini pia wako sokoni kusaka beki wa kati na walirusha ndoano kwa Rugani, ambaye alishindwa kujihakikishia namba kikosini Juventus tangu aliporejea kutoka Empoli alikokuwa kwa mkopo 2015.
Arsenal walitaka kumchukua Rugani kwa mkopo wa miaka miwili na kipengele cha kumnunua jumla mwisho wa mkopo wake.

Lakini Juventus wamekataa jambo hilo, huku mabingwa hao wa Serie A wakisema hawako tayari kumtoa beki huyo mwenye umri wa miaka 25 kwasababu wanataka kuingia katika msimu huu mpya wakiwa na mabeki wa kati watano kwani pia kuna shaka kuhusu uzima wa Giorgio Chiellini.

Rugani pia ana furaha kubaki Turin, whuku akidhamiria kufanya kazi na kocha mpya Maurizio Sarri – ambaye alikuwa na uhusiano naye mzuri alipokuwa kocha wa Empoli.

Jambo hilo linailazimisha Arsenal kuangalia kwingineko huku muda wa dirisha la usajili ukielekea ukingoni. Litafungwa Alhamisi hii Agosti 8.

Arsenal ilimsajili beki wa kati William Saliba, 18, lakini imemrejesha kwenye klabu yake ya St Etienne ya Ufaransa ili akapate uzoefu zaidi. 

Pia imevunja rekodi yake ya usajili kwa kunasa saini ya winga kutoka Lille, Nicolas Pepe, kwa Pauni 72 milioni na imemchukua kiungo Dani Ceballos kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Real Madrid na pia imemnasa winga Martinelli kutoka Brazil kwa Pauni 6 milioni. 


EmoticonEmoticon