Arsenal Yamuuza Laurent Koscielny

Arsenal wamemuuza beki wao wa kati na nahodha Laurent Koscielny kwa klabu ya Bordeaux kwa dau la Euro milioni 5.
Mchezaji huyo mwenye miaka 33 anarejea katika ligi ya Ufaransa baada ya miaka tisa ya kucheza England katika klabu ya Arsenal.
Koscielny alikuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Arsenal na klabu hiyo yenye maskani yake jijini London ilitaka mchezaji huyo aendelee kusalia klabuni hapo.
Hata hivyo, mchezaji huyo aling'ang'ania kuuzwa na kugoma kusafiri na timu kwenda kwenye ziara ya kujiandaa na msimu mpya nchini Marekani.
"Tumekubali uhamisho kwenda Bordeaux baada ya kuafikiana vyema kuhusu vigezo vya usajili," imeeleza Arsenal katika taarifa yake.
"Tunamshukuru Laurent kwa mchango wake katika klabu hii na tunamtakia kila la kheri katika maisha yake ya baadae."
Koscielny alikataa mkataba mpya na Arsenal, maarufu kama Gunners baada ya kuona kuwa vipengele vya mkataba huo vinadogosha mchango wake na uwezo wake wa baadae klabuni hapo.
Arsenal tayari ilishaanza kuchukua hatua za kinidhamu juu ya mgomo wa nahodha wake huyo na kwanza walimtaka kufanya mazoezi na wachezaji wa chini ya miaka 23. Hata hivyo baadae walimruhusu kuendelea na maandalizi na timu ya wakubwa kwa ajili ya msimu mpya.


EmoticonEmoticon