Chanzo, Dalili, Changamoto Za Magonjwa Ya Akili

Wataalam wa afya wamebaini kuwa siyo watu wote wanaovuta bangi na kunywa pombe kupita kiasi hupenda kufanya hivyo. Wengine hulazimika kutokana na maradhi ya afya ya akili.  Maradhi ya afya ya akili yanaweza kumsababisha mtu kutumia mihadarati na kunywa pombe. Akili inapopata shida, mhusika husikia kelele kichwani na hutafuta mbinu za kukabiliana na hali hiyo.

Akibaini akinywa pombe hatazisikia, basi hukimbilia kunywa na akibaini kuwa akivuta bangi hatasikia karaha au usumbufu anaoupata, basi atakuwa anavuta na atafanya hivyo kila anapohisi kupata shida hiyo. 
Mara nyingi wanaume ndiyo hukimbilia mbinu hizo ukilinganisha na wanawake ambao wengi wao hufikishwa hospitalini kwa ajili ya matibabu. Magonjwa ya afya ya akili ni yale yanayoathiri uwezo wa mtu kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda katika utashi wake.

Hivyo mgonjwa anakuwa na tabia au mwenendo ulio tofauti au usioendana na jamii husika. Ikitokea mtu amevuta bangi ikamchanganya akili akafikishwa hospitalini akiwa amefungwa kamba hukaa naye akipatiwa huduma ya kwanza hadi pale nguvu ya bangi itakapokwisha.

Kama ni mvutaji wa kawaida nguvu ya bangi ikiisha anakuwa sawa na anaruhusiwa kurudi nyumbani na jambo hilo ni kawaida kabisa, lakini akiwa anavuta kwa sababu ya matatizo ya akili hata nguvu ya bangi ikiisha anakuwa hayupo sawa na hafanyi vitu vya kawaida. Bahati mbaya ni asilimia 40 ya watu wenye maradhi hayo hufikishwa hospitali, tofauti na hapo unyanyapaa husababisha wengi wao kukimbia na kuingia mitaani.

Matumizi ya pombe na dawa za kulevya mara nyingi hutumiwa kukabiliana na hali mbalimbali za afya ya akili, ikiwa ni pamoja na kutojitambua. Watu wengi wanaopata shida ya maradhi ya akili hushindwa kukabiliana nayo na hutafuta liwazo la hali hiyo, mwisho huangukia katika matumizi ya pombe na dawa za kulevya.

CHANZO CHA MARADHI YA AKILI
Zipo sababu za kibaolojia, maradhi ikiwamo Ukimwi, kifua kikuu na uraibu. Wengine tangu wamezaliwa vipashio vya mwili havijakaa sawa (neurotransimitters) ambavyo kazi yake ni kupasha habari wakati mwingine vinakuwa na tatizo, hivyo vinamuweka mtu katika hatari ya kupata maradhi ya afya ya akili.

Maradhi kama Ukimwi, malaria na kifua kikuu huweza kumuathiri mtu kulingana na namna atakavyoyapokea na kukabiliana nayo. Maradhi yanasababisha kimoja miongoni mwa maradhi ya afya ya akili ambacho ni msongo. Kwa mfano, mtu mwenye presha akifurahi inapanda, akichukia inapanda, asiposamehe inapanda, hivyo anakuwa kwenye hatari ya kupata maradhi ya afya ya akili.
Sababu nyingine kuwa ni ya kisaikolojia. Kila binadamu ana nafsi, mambo ya kiroho ambayo hayashikiki yanavyofanya kazi kama huna nafsi wewe siyo mtu, hiyo nafsi huwa inalelewa kuanzia tumboni hadi kukua ili kutambua mambo, kutafsiri mazingira yake na kukabiliana na changamoto za maisha kama vile watu wanavyotaka ukabiliane nazo. Kwa mfano jinsi mtu anavyokabiliana na misiba, kukosa kazi, hivyo kama saikolojia yake tangu anakuwa haikulelewa vizuri atakuwa kwenye hatari ya kupata maradhi ya afya ya akili.

CHANGAMOTO
Changamoto duniani kote zinatoka kwenye mazingira. Umaskini kupita kiasi ni changamoto ngumu kuikabili kisaikolojia, lakini wanaoweza kukabiliana nayo wanaishi kitajiri kuliko matajiri wenyewe. Hivyo umaskini ni jinsi ambavyo mhusika anautafsiri, kila mmoja anavyotafsiri umaskini inawezekana mtu ana vitu ambavyo mwingine hana na akajiita maskini akapata msongo wa mawazo na hata kutamani kujinyonga.

Changamoto nyingine ni migogoro isiyokwisha kwenye jamii inayomzunguka, kazini, nyumbani na kwenye nyumba za ibada. Pia katika jamii ambayo inaamini mwanamke asipoolewa hana maana na haheshimiki ni changamoto. Changamoto nyingine ni aina ya maisha ikiwamo ulevi na ulaji usiozingatia taratibu.

DALILI
Kuna dalili kubwa tano za maradhi ya afya ya akili ikiwamo kuhisi, kugusa, kuona, kusikia na kunusa. Wapo wanaohisi kuwashwa, kutembewa na vitu ambavyo havipo au kuhisi anakimbizwa.Kuna watu wengine wakila chakula huhisi harufu tofauti na iliyopo, muda wote wakila wanatema.

Hisia potofu ni pamoja na imani za ajabu ambazo haziendani na mila, tamaduni au desturi za jamii kama vile yeye ni mtu maarufu au anaamini kuwa yeye ni nabii au bila yeye hakuna kitakachofanyika. Anaweza kusema fulani ananiloga, hilo halina shida, lakini ili ujue kuwa akili ina shida matendo atakayoyafanya kuhusu madai hayo ndiyo yatakupa jibu kuhusu utimamu wa akili.

Wapo wanaohisi kuwashwa na kutembewa na vitu ambavyo havipo. Kwa mfano wanaotumia mihadarati muda wote wanajikuna kama kuna vitu vinawatembea, kiuhalisia hakuna kitu kinachowatembea wala kuwawasha hivyo mtu anapokuwa na dalili hizi anakuwa na matatizo ya akili hivyo ni vyema kufikishwa hospitali ya karibu ili kuanza tiba mara moja.


EmoticonEmoticon