Hatua Nne Za Kutambua Maambukizi Ya Ukimwi


Ugonjwa wa HIV/AIDS umekuwa janga kubwa sana duniani kwa sasa kutokana kuathiri watu wengi na kukosekana kwa tiba ya ugonjwa huu. Maambukizi ya ugonjwa wa HIV/AIDS hufahamika kama maambukizi ya VVU (Virusi vya Ukimwi). Mtu anapopata magonjwa nyemelezi (opportunistic infections) ndiyo huwa tunasema mtu amepata ugonjwa wa UKIMWI au AIDS.  Natumai kwa kupitia makala haya tutakuwa tumetoa mwanga kidogo wa hatua za ugonjwa wa VVU. Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani ‘WHO’, kuna hatua kuu nne za ugonjwa wa VVU/UKIMWI ambazo ni:

HATUA YA KWANZA (PRIMARY HIV INFECTION)
Hatua hii huwa kwa muda wa wiki nne. Ni asilimia 20 tu ya watu wenye maambukizi ya VVU walio kwenye hatua hii ambao hupata dalili na viashiria vikali vya ugonjwa huu lakini mara nyingi madaktari hushindwa kutambua kama mgonjwa amepata maambukizi ya VVU kutokana na dalili na viashiria vyake hapa kufanana sana na dalili za magonjwa mengine.

Mgonjwa aliye katika hatua hii ya kwanza ya maambukizi ya VVU huweza kuonesha dalili na viashiria kama vile kuvimba tezi, kupatwa na homa kali, kuumwa koo, kujihisi mchovu, kujihisi maumivu sehemu mbalimbali mwilini, kutokwa na vipele mwilini na pia kutapika, kuharisha au kuumwa tumbo.
Mgonjwa anayepata dalili na viashiria hivi tunasema kwamba amepata “Acute HIV infections.” Dalili hizi hutokana na mwili wa mtu mwenye maambukizi ya VVU kuanza kutengeneza kinga dhidi ya VVU.

HATUA YA PILI (CLINICALLY ASYMPTOMATIC STAGE)
Katika hatua hii ambayo inaweza kudumu kwa muda wa miaka kumi, mgonjwa anakuwa haonyeshi dalili/viashiria vyovyote vile isipokuwa anaweza kuwa na tezi zilizovimba. Kiwango cha VVU kwenye damu hupungua sana lakini mgonjwa anaweza kuambukiza mtu mwingine yoyote na vipimo vya VVU vina uwezo wa kutambua uwepo wa maambukizi ya VVU katika damu.

Katika hatua hii VVU katika mwili huwa bado zinazaliana na hukimbilia/hujificha kwenye tezi. Kutokana na kujificha kwake katika hatua hii, kipimo cha kupima wingi wa virusi vya ukimwi katika mwili hutumiwa sana ili kuweza kutambua uwepo wa VVU.

HATUA YA TATU (SYMPTOMATIC HIV INFECTION)
Kutokana na kuongezeka kwa wingi wa VVU katika mwili, kinga ya mwili huzidi kudhoofika na hii husababishwa na; Tezi na tishu zilizoathiriwa na VVU huharibika kutokana na maambukizi ya muda mrefu. VVU hubadilikabadilika na kuwa na uwezo zaidi wa kuathiri tishu na sehemu mbalimbali za mwili na hata kuziua/kuziharibu seli zinazokinga mwili kutokana na maambukizi zinazojulikana kama T helper cell na kushindwa kuzalisha seli nyingine mpya.

Dawa za kufubaisha VVU au Antiretroviral therapy (ARV’s) huanza kutumiwa wakati seli aina ya CD4 zinapopungua na kuwa kiwango cha chini sana. Kupungua kwa seli hizi za CD4 ni kielelezo cha kinga ya mwili kuwa dhaifu. Matumizi ya dawa hizi huboresha kinga ya mwili na kumfanya mgonjwa kuishi kwa muda mrefu bila kuonyesha dalili au viashiria vyovyote vile.

Kama mgonjwa wa VVU hatumii dawa za kufubaisha VVU au anatumia ARV’s ambazo hazimsaidii au hazifanyi kazi vizuri mwilini mwake, basi mgonjwa ataendelea kuingia kwenye hatua ya nne ya Ukosefu wa Kinga Mwilini (Ukimwi) au AIDS.

HATUA YA NNE (UKIMWI)
Kama nilivyoeleza hapo juu, hatua hii hujulikana kama Ukosefu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) au AIDS, ambapo mgonjwa hupata maambukizi ya magonjwa nyemelezi pamoja na saratani za aina mbalimbali kutokana na kupungua kwa kinga mwilini.

Kwa watu wazima na watoto walio na umri zaidi ya miaka mitano, uwepo wa ugonjwa wowote nyemelezi pamoja na kushuka kiwango cha CD4 chini ya 200 cells/mm3 au kushuka kwa seli za CD4 chini ya asilimia 15 hutambulika kama ugonjwa wa Ukimwi.

Kwa watoto walio chini ya miaka mitano, uwepo wa ugonjwa wowote nyemelezi/ kushuka kwa seli za CD4 chini ya asilimia 20 kwa wale wenye umri kati ya miezi 12-35 hutambulika kama wana ugonjwa wa Ukimwi. Watoto wenye umri chini ya miezi 12, kupungua kwa seli za CD4 chini ya asilimia 25 ndiyo hutumika kutambulisha wana ugonjwa wa Ukimwi.

USHAURI
Ukiona dalili hizo wahi kamuone daktari wako.


EmoticonEmoticon