Lukaku Anukia Inter Milan

Inter Milan wapo katika hatua za mwisho za kumsajili mshambuliaji wa Manchester United Romelu Lukaku baada kuongeza dau la usajili.
Mwezi Julai, United ilikataa dau la pauni milioni 54 kwa ajili ya usajili wa Lukaku kwenda Inter.
Lukaku pia amepigwa faini na United baada ya kukicha mazoezi ya timu hiyo bila ruhusa ya uongozi.
Mchezaji huyo amekuwa akifanya mazoezi na klabu yake ya zamani Anderlecht kwa siku mbili zilizopita.
Ajenti wa Lukaku, Federico Pastorello, alilazimika kwenda jijini London jana ili kukutana na wawakilishi wa Man United ili kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Usiku wa Aug 07, Pastorello alituma picha katika mtandao wake wa Instagram akiwa kwenye ndege na Lukaku na kuandika maelezo yafuatayo: "Tayari kwa kupaa. Muelekeo Milano."
 
Inter na United wamekuwa wakivutana juu ya thamani halisi ya mchezaji huyo, huku United ikitaka walau kurejesha pauni milioni 75 ambazo walitumia kumsajili miaka miwili iliyopita.
Inter pamoja na mahasimu wao katika ligi ya Serie A klabu ya Juventus walikuwa ndio timu zinazominyana kuitaka saini ya mshambuliaji huyo raia wa Ubelgiji.
Romelu Lukaku amefunga magoli 42 katika mechi 96 alizoichezea Man United.
Kocha wa Inter, Antonio Conte alitangaza toka awali kuwa Lukaku ndiye kipaumbele chake cha kwanza kwenye dirisha hili la usajili. "Ninamchukulia kama mchezaji ambaye anaweza kuboresha kikosi chetu," amesema Conte.


EmoticonEmoticon