Mambo 10 Yanayosababisha Ugumba Kwa Mwanawake


Ugumba ni hali ya wapenzi au mke na mume kutopata ujauzito. Ugumba unaweza kuwa primary infertility yaani mtu hajawahi kubeba mimba kabisa tangu azaliwe au secondary infertility yaani mtu ambaye amewahi kuzaa lakini kwa sasa ameshindwa kubeba ujauzito.  

Utafiti unonyesha kuwa katika kila ndoa tano au uhusiano wa kimapenzi basi uhusiano mmoja una matatizo ya uzazi wa kushindwa kuzaa. Hali hii imekuwa ikiongezeka kadiri miaka inavyosonga mbele kwa sababu mbalimbali kama mionzi ya mawasiliano yaani wi-fi, magonjwa mapya ya binadamu na kadhalika.

Kwa wanawake utafiti mpya unasema uwezo wao wa kubeba mimba unaanza kupungua baada ya miaka 30 ya umri kutokana na kuanza kuishiwa nguvu kwa viungo vya uzazi. Ugumba una vyanzo vingi sana ambavyo vingine havifahamiki mpaka leo lakini hebu tuone vyanzo muhimu vya ugumba kama ifuatavyo.

1.UTOAJI MIMBA
Huenda hiki kitakuwa chanzo kikuu cha ugumba, siku hizi wanawake wengi wana sababu za kutoa mimba, utoaji wa mimba una hatari nyingi ambazo huweza kuleta ugumba kama kuoza au kuharibika kwa kizazi baada ya kushambuliwa na bakteria, makovu yanayoletwa na vifaa vinavyotumika kutoa mimba kwenye mfuko wa uzazi na mlango wa uzazi huweza kusababisha ugumba usiotibika.

2.MATATIZO YA VIZALISHAJI VYA MAYAI (OVARY)
Ovari ni kiungo ambacho kinatoa yai moja kila mwezi ili liweze kurutubishwa na mbegu ya mwanaume lakini kuna magonjwa ambayo yanaweza kusababisha ovari hiyo ikaugua na kushindwa kutoa mayai. Mwanamke ana ovari mbili lakini moja ikiugua tu na nyingine haifanyi kazi mfano ugonjwa wa ovarian cyst.

3.MATATIZO YA MIRIJA YA UZAZI
Ovari zimeunganishwa kwenye mirija ambayo hupitisha mayai kwenda kwenye mfuko wa uzazi. Wakati mwingine mirija hiyo huziba kwa sababu mbalimbali hivyo mayai hushindwa kupita na kusababisha ugumba, mfano ugonjwa wa endometriosis au kufanyiwa upasuaji na peritonitis.

4.MATATIZO YA UZAZI
Kizazi ndiyo sehemu kuu ambayo mtoto hutunzwa na kuishi kwa miezi yote tisa, tatizo lolote linaloshambulia kizazi huleta ugumba. Kwa mfano, makovu ndani ya kizazi, uvimbe ndani ya kizazi, kugeuka kwa kizazi na magonjwa ya zinaa kama  kaswende na kadhalika husababisha kizazi kisiweze kutunza mimba.


5.KANSA YA KIZAZI
Kansa ya kizazi huzuia yai la mama lililorutubishwa kushindwa kujiweka kwenye mfuko wa kizazi ili kukua, hivyo huchangia sana mimba kuharibika au kutotungwa kabisa.

6.MATATIZO YA MLANGO WA KIZAZI
Oparesheni za kizazi, utoaji wa mimba na magonjwa ya zinaa huweza kusababisha kuziba kwa mlango wa uzazi hivyo mbegu za kiume kushindwa kabisa kupita kwenye mlango wa uzazi na kusababisha ugumba.

7.MAGONJWA MENGINE
Magonjwa yoyote ya binadamu ambayo huingilia mfumo wa homoni za uzazi huleta ugumba mfano magonjwa ya ini, kisukari, hyperthyrodism na kadhalika.

8.MATUMIZI YA SIGARA, POMBE
Unywaji wa pombe kupita kiasi na uvutaji wa sigara au bangi huzuia yai kutoka kwenye ovary. Uvutaji wa sigara hupunguza uwezo wa yai kutembea kutoka kwenye ovari kwenda kwenye mfuko wa uzazi na wakati mwingine husababisha mimba kutunga nje ya kizazi.

9.MSONGO WA MAWAZO
Ukiwa unatafuta mtoto tayari ukiwa umepaniki kwamba huenda usimpate husababisha mwili kutoa homoni kitaalamu huitwa cortisol ambazo huzuia kazi za homoni za uzazi ambazo kitaalamu tunasema gonadotrophin releasing hormone hivyo hali huzidi kuwa mbaya na mama kushindwa kushika mimba.

10.UNENE MKUBWA
Mwili mkubwa unaingilia mfumo wa utengenezaji homoni za uzazi hivyo huweza kuleta ugumba katika umri mdogo sana wa mwanamke. Hivyo basi,kupunguza uzito ni moja ya njia bora kabisa ya kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuzuia ugumba na kupata mimba.

USHAURI
Kabla hujaanza kuzunguka kwa waganga wa kienyeji na mahospitalini ni bora kujichunguza kama uko kwenye hatari zilizotajwa hapo juu. Kama una tatizo lolote kati ya hayo tuliyoyataja mtafute mtaalamu wa afya akuchunguze kisha atakusaidia na hatimaye utapata mtoto.
Hakuna dawa moja ambayo ina uwezo wa kutibu ugumba kwa watu wote bila kutibu chanzo chake kwanza, hivyo ukimuona daktari akasikiliza historia ya maisha yako na chanzo cha tatizo lako anaweza kukupa dawa na ukazaa.


EmoticonEmoticon