Tatizo La Ugumba/Utasa Kwa Mwanaume


Tatizo la ugumba limekua kubwa na umefika wakati lizungumzwe kwa kuangalia upande wa pili wa shilingi.
Inaelezwa kuwa katika kila ndoa sita, moja huhangaika kupata uzazi na mmoja kati ya wawili hao anaweza kuwa mgumba.

Zipo sababu mbalimbali zinazochangia ugumba kwa wanaume ikiwamo matatizo ya kuzaliwa nayo au kuyapata ukubwani ikiwemo magonjwa mbalimbali. 
Matatizo yafuatayo yamekuwa ndiyo mara kwa mara chanzo cha kujitokeza kwa tatizo la ugumba kwa wanaume. 

Yako mambo yanayosababisha utengenezaji wa mbegu zisizo na ubora zinazokosa ufanisi wa kazi yake. Mambo hayo ni pamoja na kuzaliwa na korodani ambazo hazijashuka kutoka tumboni.
Kwa kawaida, kabla ya kuzaliwa kokwa za kiume huwa zipo ndani ya pango la tumbo na hutakiwa zishuke kuelekea sehemu za uzazi baada ya kuzaliwa. 
Kushindwa kushuka na kuhifadhiwa katika korodani husababisha mbegu au kokwa kuharibika kutokana na joto kali la tumboni. 
Kushuka na kuning’inia kwa korodani ni maumbile sahihi ya kibailojia yenye tija kiafya ambayo huwezesha kupata joto la wastani hivyo kutengenezwa mbegu zenye kiwango.

Matatizo kwenye mfumo wa chembe za urithi. Mwanadamu anaweza kurithi chembe za urithi zenye maelekezo ya kimwili yasiyo ya kwaida hivyo kujikuta akizalisha mbegu zisizo na ubora. 
Maambukizi ya virusi hatari ikiwamo virusi vya mumps na maambukizi sugu ya magonjwa maeneo ya uzazi, huchangia ugumba kwa mwanaume.

Ajali za bahati mbaya zinazotokea wakati wa upasuaji wa kurekebisha matatizo ya kiafya ikiwemo katika korodani au ngiri (hernia) na aina ya kizamani ya upasuaji wa tezi dume. Hili pia huchangia tatizo la ugumba kwa wanaume. 
Kuwahi kuasiliwa na kufungwa kitanzi katika mrija kama njia za uzazi wa mpango husababisha ugumba.

Kuongezeka ukubwa wa mishipa inayorudisha damu mwilini kutoka katika korodani au kokwa huweza kusababisha damu kwenda kwa kasi eneo hilo na kuongeza joto hivyo kuathiri ufanisi wa utengenezaji wa mbegu hizo ikiwemo wingi wake na maumbile.
Uwepo wa vizuizi katika utolewaji wa mbegu za kiume huweza kuwa na tatizo. 
Matatizo ya kujamiiana ikiwemo wanaume kuwa na tatizo la kutoa mbegu haraka isivyo kawaida wakati wa tendo. 

Tatizo la mbegu kuchepukia katika kibofu cha mkojo badala ya kupitia katika mrija wa mkojo, huwa ni sababu mojawapo ya ugumba.
Kuugua magonjwa ya zinaa hadi kufikia madhara ya kuharibu mfumo mzima wa utengenezwaji wa mbegu za kiume, huangukia katika tatizo hili. 
Zipo baadhi ya kemikali ambazo kama mwanaume zitamwingia mwilini au kukaa katika maeneo yenye kemikali hizo kwa muda mrefu, zinaweza kumletea ugumba. 

Kemikali hizo ni kama madawa ya kilimo, rangi, mipira, mionzi na dawa za steriods.

Unywaji pombe kupindukia ni tatizo ambalo limekuwa likizidi kuwa kubwa.
Hii ni kutokana na maendeleo ya kichumi, watu wengi wamejiingiza katika unywaji wa pombe uliopindukia. Matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine, bangi, hashishi, mihadarati yote hayo hupunguza idadi na kiwango cha mbegu za kiume (sperms).

Madhara ya saratani na matibabu yake ambayo yanahusisha mionzi na kemikali tiba za saratani nazo zinaweza kuathiri utengenezwaji wa mbegu za kiume. 

Uondolewaji wa kokwa za kiume baada ya kupata saratani au uvimbe ni chanzo kingine cha ugumba au wengine wanaweza kupata ajali maeneo ya uzazi na kuwafanya wagumba.

TIBA NA USHAURI
Yeyote ambaye ana matatizo tuliyoyaanisha hapo juu anatakiwa kuonana na daktari ili apimwe na kama tatizo lake litahitaji dawa atapatiwa, lakini pia anaweza kupewa ushauri ikiwa itagundulika kuwa ana matatizo hayo.


EmoticonEmoticon