Itambue Thamini Penzi Lako Kabla Ya Kuvunjika


Nafahamu wakati unajikuta katika wakati mgumu wa kuamua hatma ya uhusiano wako na mpenzio kwa kuwa unahisi unampenda sana na kwamba hauko tayari kumkosa maishani. Labda tubadilishane mawazo kwa kuangalia namna unavyoweza kulifanyia tathimini penzi lako la sasa kabla ya kuamua kuachia ngazi;

1. Ni vizuri kabla hujaanza kulalamika kwa watu wa pembeni, hakikisha unamwambia ukweli mwenzi wako juu ya tabia yake na kumueleza ni jinsi gani unaumizwa mno na tabia hiyo. Lakini hakikisha unaongea naye katika hali ya upendo na sio kuporomosha lawama na kubwatuka hovyo, la sivyo atakugeuzia kibao na mtakosana zaidi.

2.Kwa mpenzi anayeonesha angalau kubadilika ni heri kwako, lakini kwa wale sugu ambao wanaendeleza tabia zao hata mwaka mzima na kuwa hodari sana wa; ‘samahani honey, si unajua binadamu hukosea na kujisahau, nisamehe mpenzi.’ Hivi hii ni samahani gani wakati unarudia makosa yaleyale kila kukicha, mpenzi wako akueleweje kama sio kumdharau? Ukiwa na mtu wa namna hii, mtazame vizuri kisha uamue!

3.Kuna hili la tabia yake; kuna mambo mengine madogo madogo yanaweza kuvumilika kwa kuwa huenda sio ishu sana. Lakini kuna tabia nyingine huna haja ya kuzifumbia macho na kujiongopea kuzivumilia. Kwa mfano tabia ya vipigo kila siku, utavumilia mpaka utakapotolewa macho au unyofolewe na roho yenyewe kabisa au?
Mpenzi malaya, utamvumilia mpaka pale atakapokuletea Ukimwi uhangaike nao? Sidhani kama ni busara kuvumilia haya, usikubali kabisa kupelekwa pelekwa na hiyo hisia yako ya ‘lakini nampenda sana!’ Hebu jiangalie vizuri.

4.Wakati mwingine ni vyema sana ukawaomba watu ushauri juu ya nini ufanye unapokabiliwa na msongo wa mawazo unaotokana na kero za mpenzi wako. Kwa wanandoa wanaweza kuwahusisha wazee na wakati mwingine hata vyombo vya sheria. Usikubali kunyamaza na kumezea matatizo uliyo nayo, utakufa kihoro buree! Waombe ushauri wale unaowaamini huenda wakakuonesha njia.

5.Jifunze kwa wengine. Jiulize, hivi ni wangapi unaowafahamu na wengine kusikia habari zao, ambao waliwahi kupenda kama wewe lakini kutokana na manyanyaso na kutosikilizana wameachana na wapenzi wao, na sasa wanaishi maisha mengine matam na wapenzi wao wapya, kwa nini usiwe wewe?

6.Kumbuka kauli ya ‘siwezi kuishi bila yeye’ ni minyororo na kufuli nzito unayojifungia nayo katika jela yako wewe mwenyewe. Hebu jaribu kupigana kiume na mawazo haya na ujiweke huru. Hakuna anayeshikilia pumzi ya mwingine!

7.Pamoja na yote, ukweli unabaki palepale kwamba kuamua, kummwaga mtu unayempenda si kazi ndogo, lakini inafikia mahali inakuwa haina jinsi inakubidi. Uwe jasiri ili uondokane na maisha ya roho juu juu kila siku! Potelea mbali ili mradi upate uhuru wa nafsi.

8. Amini kuwa huenda Mungu hakukupangia ufurahi maisha na huyo uliye naye sasa kwa kuwa yule wako original bado yu njiani na kusahau machungu yaliyopita Inshaallah!


EmoticonEmoticon