Usajili Wa Mbappe, CR7 & Neymar Umelipa Katika Vilabu Vyao?

Katika uchizi huu wa kutumia pesa nyingi kununua wachezaji, tumeshuhudia baadhi ya nyota walionunuliwa kwa mkwanja mrefu wakichemsha vibaya huku wengine wakithibitishwa ubora wao.
Aidha, ulimwengu wa soka pia umeshuhudia mastaa ambao licha ya wengi kuamini hawakustahili kununuliwa kwa fedha nyingi kama dunia inavyoshangazwa na stori ya Maguire, lakini baadaye walionyesha kiwango kikubwa tofauti na matarajio ya wengi. Hawa hapa ni nyota 3 ambao usajili wao umelipa.
1. CRIASTIANO RONALDO KWENDA JUVENTUS
Licha ya kutajwa kama mmoja wa miujiza iliyowahi kushuhudiwa kwenye ulimwengu wa soka, ni ukweli usiopingika kuwa hakuna mtu aliyefikiria kungetokea klabu ambayo ingekubali kutoa zaidi ya Euro 100 milioni kwa ajili ya saini ya Cristiano Ronaldo, mwenye umri wa miaka 34.
Lakini Juventus walithubutu kumuamini Jorge Mendez, wakaingia benki na kuibuka na Euro 117 milioni, na bila hofu wakamkabidhi Mendez. Huu ulionekana kama uchizi na kufuru iliyovuka mipaka.
Lakini Mreno huyo, mshindi wa ubingwa wa Ulaya na Ballon d’Or mara tano ameonyesha uwezo mkubwa na kuwa nguzo ya Juve kuendelea kutawala Serie A.
2. KYLIAN MBAPPE KWENDA PSG
Pamoja na ukweli kwamba Kylian Mbappe alikuwa ni mmoja wachezaji walioshangaza dunia katika msimu wa 2016-17, lakini hakuna mtu ambaye angefikiria kutoa kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya saini yake kama walivyofanya PSG.
Wafaransa hao walitoa Euro 180 milioni kumsajili kinda huyo wa chini ya miaka 20. Miaka miwili baadaye kila mtu pale Paris Saint-Germain anafurahia kipaji chake. Kwa sasa ni mmoja wa wachezaji bora, ghali na wanaowindwa zaidi duniani. Mbappe ni muujiza mwingine uliotokea kwenye soka baada ya Messi na Ronaldo.
3. NEYMAR KWENDA BARCELONA
Wakati ambapo timu nyingi za Ulaya zilikuwa katika harakati za kutafuta vipaji vya soka kutoka Amerika Kusini ndipo kipaji cha Neymar kilipokuwa kinachipukia. Wakati huo akiwa bwa’mdogo mwenye ndoto za kwenda Ulaya, kila mtu alikuwa anamfuatilia.
Wakati huo moyoni Neymar alikuwa na hamu ya kuvaa jezi za Real Madrid na Barcelona. Mwisho wa siku Mbrazil huyo bishoo aliamua kutua Camp Nou katika moja ya dili za uhamisho zilizogonga vichwa vya habari duniani.
Dau lake lilikuwa ni Euro 43 milioni, baadaye ripoti zilisema dau hilo lilipanda hadi Euro 100 milioni. Kiasi hicho kilikuwa ni kufuru kutumika kwa ajili ya saini ya kinda wa miaka 21 - tena kutoka nje ya Bara la Ulaya.
Hata hivyo, fasta Neymar aliuthibitishia umma kuwa Barcelona hawakukosea kumnunua kwa kiasi hicho cha fedha. Aliisaidia Barcelona kutwaa mataji mawili ya La Liga na Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mmoja katika kipindi alichokuwa Camp Nou.


EmoticonEmoticon