Eti Hazard Ni Chibonge?

Eden Hazard
Eden Hazard maisha yake huko Real Madrid yameanza kwa kasi ya taratibu sana kiasi cha kuwafanya mashabiki waanze kumtania kwenye mitandao ya kijamii.

Staa huyo wa Kibelgiji aliyenaswa na Los Blancos kutoka Chelsea kwa ada ya Pauni 150 milioni kwenye dirisha lililopita la usajili wa majira ya kiangazi, amekumbana na wakati mgumu huko Bernabeu akiwa hajafanya chochote cha maana tangu msimu huu ulipoanza.

Mashabiki wa Madrid sasa wamemfanya Hazard kuwa kituko kwenye mitandao ya kijamii, wakidai mchezaji huyo kwa sasa yupo bize kuhakikisha anapungua uzito, kwa sababu amekuwa kibonge tangu alipotua Bernabeu.

Hazard amefanywa kituko zaidi baada ya kuonyesha kiwango cha hovyo kwenye Madrid derby huko Wanda Metropolitano, wakati Madrid ilipotoka sare ya bila kufungana na Atletico Madrid juzi Jumamosi usiku.
Eden Hazard
Mashabiki wa Real Madrid wamedaiwa kuwa watukutu sana kwa wachezaji wao, ambapo waliwahi kumzomea Cristiano Ronaldo licha ya kufanya vyema na kuvunja rekodi kibao kwenye kikosi hicho cha Los Blancos.

Staa wa Wales, Gareth Bale amekuwa kwenye wakati mgumu wa kuwashawishi mashabiki wa timu hiyo tangu alipojiunga nayo mwaka 2013 na wasiwasi umeibuka kuhusu Hazard, ambaye pia anaweza kujikuta kwenye wakati mgumu kama atashindwa kuonyesha kiwango bora ndani ya kipindi kifupi kijacho.

Kocha wa zamani wa Chelsea, Glenn Hoddle hivi karibuni aliwahi kusema Hazard amekwenda kujiunga na Real Madrid katika kipindi kigumu.


EmoticonEmoticon