Lukaku Akunjana Mashati Na Mwenzake

Straika Romelu Lukaku na mchezaji mwenzake wa Inter Milan, Marcelo Brozevic wameripotiwa kukunjana mashati kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kabla ya wenzao kuwagombelezea kufuatia kupishana lugha juu ya mchezo wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Inter Milan iliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Slavia Prague kwenye mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambapo Nicolo Barrella alipiga bao la kusawazisha katika dakika za majeruhi.

Kwa mujibu wa La Gazzetta dello Sport, Lukaku aliwakosoa wenzake kwa kushindwa kufuata mbinu za Kocha Antonio Conte kwenye mchezo huo wa Jumanne iliyopita, jambo ambalo lilimfanya Brozovic ashindwe kuvumilia kutokana na maneno ya Mbelgiji huyo.

Taarifa zinabainisha kulikuwa na vuta nikuvute kabla ya wachezaji wengine kuingilia kati kabla ya mambo kuharibika zaidi. Inter itakipiga na mahasimu wake, AC Milan kesho Jumamosi na hapo ndio inaelezwa msimu wao utakuwa unaanza rasmi.

Lukaku anajaribu kuondokana na nyakati ngumu tangu alipotua Inter Milan kwa ada ya 74 milioni akitokea Manchester United baada ya kusemwa kwamba alikuwa na uzito mkubwa wakati alipokuwa akiwasili huko San Siro.

Mbelgiji huyo alikutana na nyakati ngumu pia za kubaguliwa kwa rangi yake na mashabiki wa Cagliari alipokutana nao kwenye mchezo wa Serie A.

Kwenye Serie A msimu huu, Lukaku tayari ameshafunga mabao mawili katika mechi tatu.


EmoticonEmoticon