Maneno Ya Kujitete Ya Kocha Wa Man United

Ole Gunnar Solskjaer
Ole Gunnar Solskjaer anasisitiza kwamba yeye ni mtu sahihi wa kuiongoza Manchester United, licha ya kwamba timu yake ipo alama tatu tu juu ya mstari wa kushuka daraja.
Tangu Solskjaer apewe rasmi usukani wa kuinoa klabu hiyo mwezi Machi, Man United wameshinda mara tano tu katika mechi 18.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 46, anapigiwa upatu kuwa miongoni mwa makocha wawili wa ligi ya Primia waliopo kwenye hatari ya kupoteza ajira zao muda wowote pamoja Marco Silva wa Everton .
"Mimi mwenyewe sina wasiwasi, kama sitajiamini mwenyewe basi dunia yote itakosa imani nami" amesema kocha huyo.
United inatarajia kucheza na Arsenal usiku wa leo baada ya kupoteza mechi ya nyumbani dhidi ya Crystal Palace na ugenini dhidi ya West Ham katika msimu huu.
Klabu ipo nyuma ya vinara Liverpool kwa pointi 13 na kuwa na pointi tatu tu mbele ya Aston Villa iliyopo nafasi ya 18, ambayo ndipo mstari wa kushuka daraja huchorwa.
"Tulikuwa na mjadala mkubwa sana, lakini tunaamini kile tunachokifanya," alisema Solskjaer
Mechi dhidi ya Arsenal inakuja siku chache baada ya kuondoka kwa kocha wa walinda mlango Emilio Alvarez.
Alvarez, ambaye alikuwa na uhusiano mzuri wa kazi na David de Gea tokea klabu ya Atletico Madrid, alipoteza nguvu yake baada ya klabu hiyo kumleta Richard Hartis kuwa kocha mkuu wa magolikipa hivi karibuni.
Hartis, alishawahi kufanya kazi klabuni hapo kwa mwongo mmoja na awali alifanya kazi na Solskjaer huko Molde na Cardiff.


EmoticonEmoticon