Sababu Iliyomfanya CR7 Kumwaga Machozi Kwenye Mahojiano Ya Televisheni

Cristiano Ronaldo Akilia na Kupangusa Machozi
Cristiano Ronaldo, amesema hakutarajia kulia katika televisheni kufuatia mazungumzo yaliyomuhusisha baba yake Jose Dinis Aveiro.

Mshambuliaji huyo wa Juventus alimwaga chozi  katika kipindi cha mtangazaji Piers Morgan.

Ronaldo alilia alipoonyeshwa video ya baba yake ambaye awali hakuwahi kumuona.

Video hiyo ilimuonyesha Aveiro akizungumzia Fainali za Kombe la Ulaya zilizofanyika mwaka 2004 nchini Ureno.

Nahodha huyo wa Ureno alishindwa kujizuia alipomuona baba yake ambaye alifariki mwaka 2005 Ronaldo akiwa na miaka 20.

Askari huyo wa zamani, alifariki akiwa na miaka 52 kutokana na maradhi ya ini yaliyosabishwa na unywaji mkubwa wa pombe.

‘Sikutarajia kama ningelia. Kamwe sikuwahi kuona video hii,” alisema Ronaldo.

Ronaldo alikiri kutomfahamu baba yake kwa asimilia 100 kwa kuwa aligubikwa na unywaji pombe kupita kiasi.

“Simfahamu baba kwa asilimia 100. Alikuwa mtu mlevi, kamwe sikuwahi kuzungumza naye katika mazingira ya kawaida,” alisema Ronaldo.

Baba huyo amefariki akiwa hajaona mafanikio ya Ronaldo (34), mwenye watoto wanne, mchezaji bora mara tano wa dunia na kuiongoza Ureno kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 2016.


EmoticonEmoticon