Fahamu Kuhusiana Na Saratani Ya Matiti Kwa Wanaume

“Kawaida wanaume hawana matiti, lakini yangu ninayo kidogo. Kwa hiyo huwa nashituka kwamba mwanaume anaweza kupata saratani ya matiti,” anasema Mosses Musonga katika mahojiano na BBC kuhusu ugonjwa huo.

“Lakini niligundua kuwa na ugonjwa wa saratani ya matiti mwaka 2013. Nilikuwa na uvimbe kwenye titi langu la kulia nikaenda kwa daktari, akachukua sampuli wakapeleka kwa wataalamu kufanya utafiti wakathibitisha kwamba nina saratani ya matiti. 

“Kama mwanaume ukiwa na uvimbe kwenye matiti, usipuuze kwa sababu si kawaida mwanaume kuwa na uvimbe kwenye matiti.”

Saratani ya matiti huwapata zaidi wanawake, lakini habari mpya ni kwamba hata wanaume wanaweza kuupata ugonjwa huo ingawa ni kwa kiwango kidogo.

Daktari bingwa wa saratani, Sikudhani Muya anasema Saratani ya matiti kwa wanaume ni aghalabu, inaweza kutokea ukapata mgonjwa mmoja kwa miaka 10, lakini wanawake ni tatizo linalowasumbua zaidi.

Anasema wanaume huchelewa kujigundua kutokana na maumbile yao, hivyo kufika hospitali wakiwa katika hatua mbaya.

“Wengi wanajua saratani ya matiti ni kwa wanawake pekee, ukweli ni kwamba hata wanaume wanaweza kuwa na tatizo hili. Inaweza kuwa ngumu kwao kugundua haraka kwa sababu matiti yao hayana nyama,” anasema. 

Anaeleza kuwa hali hiyo husababisha kushindwa kuona dalili kwa haraka ingawa wakipimwa wanaweza kubainika kuwa na tatizo hilo.

Anawashauri wanaume kuwa na utamaduni wa kujichunguza matiti kubaini kama kuna viashiria vya ugonjwa huo.
Naye Dk David Rita anasema kila mtu anatakiwa kujua matiti yake yalivyo, hivyo kukiwa na mabadiliko kama uvimbe, kubadilika rangi ama kutokwa na maji atambue mapema na kuwahi matibabu.

Anasema saratani zote zinatibika ikiwa mgonjwa atawahi hospitali na kupatiwa ufumbuzi katika hatua za awali.
Anasema karibu asilimia 95 ya wagonjwa wa saratani wakiwahi na kupatiwa matibabu wanaweza kupona, lakini wakichelewa uwezekano unakuwa mdogo.

Hata hivyo, Dk Ruta anasema wagonjwa wengi hufika hospitali wakiwa katika hatua ya tatu na nne ambazo ni hatua za mwisho zinazochangia mgonjwa kutopona.

Chanzo
Dk Ruta anasema mwanaume anaweza kupata ugonjwa huo ikiwa amerithi vinasaba kutoka katika familia yake.
Pia anasema ugonjwa huibika yanapotokea mabadiliko ya ghafla katika seli (brac2) ambayo yanasababisha kuwa dhaifu, hivyo kuwa rahisi kupata ugonjwa huo.

Anataja vigezo vingine vinavyochangia ugonjwa wa saratani ya matiti kwa wanaume ni kwa wenye umri zaidi ya miaka 50, mtindo wa maisha, unene kupita kiasi na msongo wa mawazo.

Dk. Ruta anasema kutokana na hali hiyo ili kupungua uwezekano wa kupata ugonjwa huo, watu wanashauriwa kubadili mtindo wa maisha kama kuepuka kuvuta sigara na kunywa pombe pamoja na kufanya mazoezi ili kuepuka kuwa na uzito uliopitiliza.

Pia anawashauri watu kuzingatia mlo kamili na kwa wakati, huku wakijiepusha na mionzi mikali.
Kutokana na hali hiyo anawashauri wananchi kula vyakula sahihi na kwa wakati.

Kwa watu wanaofanya kazi maeneo yenye mionzi mikali, anawashauri kutumia vifaa vya kujikinga ambavyo vitawandoa katika hatari ya kupata ugonjwa huo.

Dalili
Dk. Rita anasema mtu anaweza kupata uvimbe usio na maumivu kwenye titi moja au matiti yote.
Anasema uvimbe huo unaongezeka kadri siku zinavyokwenda. Pia ngozi ya matiti huwa na rangi nyekundu au kidonda.

Pia anasema rangi ya ngozi ya titi hubadilika na kuonekana kama ngozi ya nje ya chungwa, chuchu kukunjamana na kuingia ndani na hata kutoka damu au majimaji yenye damu au rangi isiyokuwa ya kawaida kwenye titi.

Dk Ruta anawashauri wananchi wakiona uvimbe usio wa kawaida katika maeneo ya matiti na makwapa wawahi hospitali kufanyiwa uchunguzi.

Jinsi ya kujichunguza
Ili kujipima saratani mwenyewe ukiwa nyumbani au sehemu yoyote tumia moja (au zote) katika njia hizi;
Ukiwa kifua wazi huku ukijitizama kwenye kioo, nyanyua mkono juu na viganja vishikane juu ya kichwa chako.

Kisha chunguza kama kuna mabadiliko yoyote katika mlingano wa ukubwa wa matiti. Kama moja litaonekana kuwa kubwa zaidi ya jingine basi ni moja ya viashiria vya athari ya saratani.

Njia nyingine ni kusimama wima na kunyanyua mkono wa kushoto juu huku vidole vya mkono wako wa kulia vikiwa vinabinya na kuachia kwa mzunguko kwenye titi kuangalia kama ndani kuna uvimbe.

Baada ya kumaliza kwa titi la kushoto fanya hivyo kwa titi la kulia. Njia hii pia hufanya ukiwa umelala chali.
Zoezi hilo linapaswa kufanyika mara kwa mara ili kujigundua mapema na kuwahi vituo vya afya kupatiwa tiba.


EmoticonEmoticon