Bayern Munich Wammendea Mauricio Pochettino

Mauricio Pochettino
Bayern Munich wameonekana kuwa siriasi katika dili la kumnasa aliyekuwa Kocha wa Tottenham Hotspurs, Mauricio Pochettino.

Habari za kuaminika zinasema kwamba, mabosi wa Bayern Munich wamepanga kukutana na Pochettino kujadili mpango wa kumpa timu japo anaweza kukutana na upinzani kutoka kwa Erik ten Hag, ambaye anainoa Ajax kwa sasa.

Hata hivyo, kabla ya mabosi hao wa Bayern kumuita Pochettino mezani kujadili mpango huo, kikao cha mabosi kitaketi ili kupata mwafaka wa pamoja na kuwajadili makocha ambao, wangependa kuwaletea Bavarian.

Pochettino, ambaye ametimuliwa kazi wiki iliyopita na Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy, kwa sasa amekuwa akiwindwa na vigogo vya soka Ulaya ikiwemo Real Madrid, Manchester United na Arsenal.

Nafasi yake baada ya kufutwa kazi imechukuliwa na kocha wa zamani wa Manchester United, Jose Mourinho ambaye alianza vyema kibarua chake akiipa ushindi wa kwanza Spurs ugenini dhidi ya West Ham United.

Kwa sasa Bayern iko chini ya kocha wa muda, Hans-Dieter Flick, ambaye ameshinda mechi tatu mfululizo huku akikusanya mabao 10 ya kufunga bila kuruhusu wavu wake kutikiswa, baada ya kufutwa kazi kwa Niko Kovac.


EmoticonEmoticon