Mambo Na Vitu Vidogo Vinavyoweza Kunogesha Penzi, Kulifanya Kuwa Lipya

Kila mmoja anapaswa kuwa furaha ya mwenzake. Anapaswa kumtendea mambo mazuri ili aweze kuwa na furaha na amani muda wote. 

Mwanaume anapaswa kushughulikia amani na furaha ya mwanamke wake, vivyo hivyo mwanamke ashughulikie furaha na amani ya mwanaume wake. 

Kuna vitu ambavyo mara nyingi huwa tunaviona ni vidogo lakini kimsingi huwa vina maana kubwa sana katika suala zima la uhusiano wa kimapenzi kwa mchumba au hata hatua ya ndoa.

MITOKO
Mara nyingi wapendanao huwa wanajisahau sana katika suala zima la mitoko ya hapa na pale. Mara nyingi kila mtu anajua kutoka kivyake na marafiki zake.

Mwanaume anatoka kwenda hoteli au sehemu mbalimbali za burudani na rafiki zake na mwanamke naye anatoka na mashoga zake. 

Ndugu zangu, hata kama kweli kila mtu ana mitoko yake lakini ni vyema kujiwekea utaratibu siku moja moja wapendanao mkatoka pamoja, ina maana kubwa sana.

ZAWADI
Lingine ni la vizawadi. Hata kama unajua kwamba mwenzako ana uwezo wa kununua kile ambacho wewe utamnunulia lakini fanya hivyo kama ishara ya upendo, inaleta maana kubwa sana katika uhusiano.

MPE KIPAUMBELE
Unapokuwa unawaza juu ya jambo fulani, mpe kipaumbele mwenzi wako kwa kuomba hata ushauri badala ya kuomba ushauri kwa marafiki zako, wafanyabiashara au wafanyakazi wenzako. 

Mwenzi wako anapoona humpi kipaumbele hususani katika masuala ya msingi, anaweza kuona ni kama unamdharau na hivyo kupunguza hamu ya kuwa na wewe.

MSAIDIE

Kuna wakati mwenzi wako anaweza kuwa anaweza kufanya jambo fulani lakini anapokuwa na wewe, anatamani wewe umsaidie, hilo nalo lina maana kubwa lifanye kadiri uwezavyo.

MJALI
Hili ni la muhimu sana, unaweza kuona kama halina maana sana lakini unapokuwa unamkumbusha mwenzi wako kuhusu suala la kula au kumuamsha asubuhi awahi kazini na mambo mengine kama hayo, yanaleta chachu na hamasa kubwa katika uhusiano.