Pata Elimu Na Ushauri Wa Sumu Inayopatikana Kwenye Vyakula, Kuharisha, Kutapika, Tumbo Kuuma.....

Food poisoning ni hali ya kuchafuka kwa chakula kunakotokana na uwepo wa vimelea mbalimbali kama vile bacteria, virusi, au parasites au sumu zao ndani yake. 

Hali hii hutokea wakati unapokula chakula au kunywa vinywaji/maji yaliyochanganyika na vimelea hawa hususani vya bacteria wa jamii ya Staphylococcus au Escherichia coli (E. coli).

Ieleweke kuwa food poisoning haimaanishi sumu inayowekwa na mtu/watu kwenye chakula bali hutokana na vijidudu vya magonjwa mbalimbali kama vile bacteria.

Matibabu
Wagonjwa wengi wa food poisoning kwa kawaida hupona kabisa baada ya siku chache tangu kujitokeza kwa dalili.

Jambo la msingi ni kuhakikisha unaendelea kula na kunywa vinywaji au maji ya kutosha ili kurejesha kiasi chochote cha maji kitakachopotea kutokana na kuharisha au/na kutapika.

Haishauriwi kula vyakula vigumu mpaka kuharisha kutakapokoma, na jiepushe kula vyakula vya jamii ya maziwa (maziwa, mtindi) ili kupunguza uwezekano wa kuharisha zaidi, wakati huo huo kunywa maji ya kutosha au vinywaji vingine kwa wingi.

Watoto wadogo ni vema wapewe maji yenye madini maalum ya ORS au kama hayapatikani, maji yenye mchanganyiko wa chumvi na sukari hufaa sana. 

Wagonjwa hususani watoto wanaoharisha na kutapika na ambao hawawezi kunywa maji wala vinywaji kwa sababu ya kutapika hawana budi kutibiwa kwa kutumia drip (i.v. fluids) ili kurejesha maji yaliyopotea.

Mara nyingi, matibabu ya food poisoning hayahusishi utumiaji wa dawa za jamii ya antibiotics isipokuwa mara chache sana daktari wako anaweza kushauri utumie dawa hizo hususani kama kunaambatana na kuharisha damu.

Nini cha kutarajia kwa mtu aliyepatwa na food poisoning?
Kwa kwaida watu wengi wenye kupatwa na hali hii hupata nafuu kamili ndani ya saa 12 mpaka siku mbili; ingawa wapo baadhi ambao hali zao zinaweza kuwa mbaya sana. 

Ni mara chache food poisoning husababisha kifo lakini kama mgonjwa anaharisha sana na kutapika bila kutibiwa, kifo kinaweza kutokea kwa sababu ya upungufu mkubwa wa maji mwilini.

Nini madhara ya hali hii?
Madhara yaliyozoeleka zaidi ya hali hii ni upungufu wa maji mwilini unaotokana na kutapika na kuharisha kupita kiasi bila kurejesha maji yanayopotea.

Madhara mengine hutegemeana na aina ya bacteria anayesababisha ugonjwa huu. 

Bacteria wengine husababisha madhara kama vile magonjwa ya figo, matatizo ya kutokwa damu bila kukoma, magonjwa ya viungo vya mwili, magonjwa ya mfumo wa fahamu, na madhara katika moyo.

Kinga ni bora kuliko tiba
Kujikinga ni bora kuliko kusibiri mpaka tatizo litokee. Unashauriwa kuepuka kula vyakula ambavyo ubora na usafi wake unatia shaka. 

Aidha epuka kunywa vinywaji au maji ambayo si safi na salama pamoja na kuacha kula nyama au samaki wasiopikwa vizuri.

Unashauriwa kwenda hospitali haraka iwapo utaona damu au usaha katika kinyesi chako, kinyesi kimekuwa cha rangi nyeusi, tumbo linazidi kusokota hata baada ya kujisaidia, kujihisi dalili za kukaukiwa maji mwilini kama vile kiu, kizunguzungu au kujihisi kichwa chepesi, kuharisha pamoja na homa kali, moyo unakwenda kasi au una dalili nyingine za tatizo hili.


EmoticonEmoticon