Barcelona, Real Madrid Vyuma Vimekaza

Watani wa jadi Barcelona na Real Madrid wametoka suluhu katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania katika mchezo uliokuwa na ulinzi mkali.

Ulinzi mkali uliimarishwa katika mchezo huo wa El Classico ambao Barcelona ilikuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Nou Camp.

Idadi kubwa ya mashabiki wa Barcelona walikamatwa jirani na uwanja huo kutokana na vitendo vya kuandama kisiasa.

Winga wa Real Madrid Gareth Bale aliweka mpira wavuni, lakini mwamuzi alikataa bao hilo kwa madai beki wa kushoto wa timu hiyo Ferland Mendy alikuwa katika nafasi ya kuotea.

Matokeo hayo yamezidisha msisimo wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu kwa kuwa timu hizo zimeendelea kulingana pointi 36, lakini Barcelona iko kileleni kwa uwiano mzuri wa idadi ya mabao.

Awali, mchezo huo ulipangwa kuchezwa Oktoba 26 kabla ya kuahirishwa kutokana na hali ya kisiasa iliyopo katika Jimbo la Katalunya inapotoka Barcelona wanaotaka kujitenga.

Jambo la kufurahisha licha ya timu hizo kuwa na upinzani mkali, zilikaa hoteli moja na zilisafiri pamoja kwenda uwanjani saa mbili kabla ya mchezo kuanza zikiwa chini ya ulinzi mkali.


EmoticonEmoticon