Mahakama Yaamua, Ukahaba Si Uhalifu

Mahakama kuu jijini Abuja imetangaza kwamba ukahaba sio uhalifu nchini Nigeria.
Uamuzi huo umejiri katika kesi iliyokuwa inashirikisha wanawake 16 waliokamatwa kwa kufanya ukahaba.
Ni mara ya kwanza kwa mahakama ya Nigeria kuamuru kuhusu uhalali wa biashara hiyo ambayo inazidi kuonekana kuwa uhalifu mkubwa miongoni mwa mataifa mengi Afrika.
Jaji Binta Nyako wa mahakama kuu ya Abuja alisema kwamba hakuna sheria inayoharamisha ukahaba nchini humo.
Kesi hiyo iliowasilishwa 2017 ilifuatia kukamatwa kwa baadhi ya wanawake mjini Abuja kwa madai ya kushiriki katika biashara hiyo.
Licha ya serikali ya taifa hilo kudai kwamba wanawake hao ni wahalifu mahakama ilipinga hilo na badala yake kuagizia kwamba walipwe fidia.
Wakili mmoja aliyekuwa akiwawakilisha wanawake hao Babatunde Jacob aliambia BBC kwamba mahakama iliamuru kwamba vyombo vya usalama vilikiuka haki za wateja wake wakati walipovunja na kuingia katika nyumba zao na kudai kwamba wanawake hao walikuwa makahaba.
Wataalam wa sheria wanaamini kwamba uamuzi huo utakuwa na athari kubwa kwa taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika.
Kukamatwa kwa makahaba na vyombo vya serikali ni kitu cha kawaida. Katika msako mmoja mnamo mwezi Mei mwaka huu, zaidi ya wanawake 60 walikamatwa mjini Abuja kwa kudaiwa kushiriki katika bishara hiyo.
Wanawake hao walidai kwamba , walinyanyaswa, kupokonywa fedha zao kwa nguvu na kuaibishwa hadharani.


EmoticonEmoticon