Tahadhari: Mvua Kubwa Kuanza Kunyesha Mikoa 14 Nchini

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari  ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika Mikoa 14 nchini.

Mikoa hiyo ni  Dar es Salaam, Pwani, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Tanga , Mbeya, Songwe, Rukwa, Iringa, Njombe, Ruvuma na kisiwani Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo inaeleza kuwa kuna uwezekano wa kutokea vimbunga pacha Magharibi mwa bahari ya Hindi upande wa Kaskazini na Kusini mwa Ikweta na kuathiri mfumo wa hali ya hewa nchini.

Inaeleza kuwa migandamizo hiyo midogo pacha inaelekea kuimarika na kuwa vimbunga katika pwani ya Somalia (upande wa Kaskazini mwa Ikweta) na Kaskazini Mashariki mwa kisiwa cha Madagascar (Kusini mwa Ikweta).

Pia,  mgandamizo mdogo wa hewa uliopo Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (karibu na kisiwa cha Madagasca) inatarajia kuimarika na kuelekea Kaskazini mwa kisiwa hicho.

Inaeleza kuwa hali hiyo itasababisha ongezeko la mvua pamoja na vipindi vya mvua kubwa  katika baadhi ya maeneo ya Pwani ya Kaskazini mwa Tanzania kati ya Desemba 5 na 6, 2019.

Kwa upande mwingine mgandamizo mdogo wa hewa katika Pwani ya Somalia unatarajiwa kuendelea kuwa mbali na Pwani ya Tanzania na hautarajiwi kuwa na madhara nchini.

CREDIT:Mwananchi


EmoticonEmoticon