Tuzo ya Ballon dOr: Messi Apigiwa Upatu kurudi Kileleni Usiku Wa Leo

Mshindi wa tuzo ya Ballon d'Or kwa mwaka 2019 anatarajiwa kutangazwa leo usiku, na kwa mara nyengine tena kwa mwaka huu Lionel Messi, Cristiano Ronaldo na Virgil van Dijk watakuwa wanachuana vikali.
Kwa kipindi cha miaka 10, tokea 2008 mpaka 2017 tuzo hiyo maarufu zaidi ya wasakata kandanda duniani ilitawaliwa na washambuliaji hatari katika kizazi cha sasa Messi na Ronaldo, kila mmoja wao akishinda mara tano.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za vyombo vya habari vikubwa barani Ulaya, kuna tetesi kuwa matokeo ya tuzo hizo yamevuja na kuonesha kuwa Messi ameshinda.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Messi anayecheza katika klabu ya Barcelona na timu ya taifa ya Argentina amepata alama 446, akifuatiwa na Van Dijk mwenye alama 382.
Mshambuliaji wa Liverpool Mohammed Salah anatajwa kuwa katika nafasi ya tatu, Ronaldo nafasi ya nne huku mshambuliaji mwengine wa Liverpool Sadio Mane akaikamilisha tano bora kwa mwaka huu.
Matokeo rasmi hata hivyo yanatarajiwa kutolewa baadae hii leo.


EmoticonEmoticon