Urusi Yafungiwa Kushiriki Michezo

Urusi imefungiwa kwa miaka minne kushiriki michezo yoyote mikubwa ya kimataifa na wakala wa kupambana na dawa za kusisimua misuli (Wada).
Inamaanisha kuwa bendera ya Urusi haitapepea wala wimbo wao wa taifa wa nchi yao hautapigwa kwenye michuano kama ya Olimpiki ya mwaka 2020 na michuano ya kandanda ya kombe la dunia ya mwaka 2022 nchini Qatar.
Lakini kwa wanamichezo ambao watathibitisha kutotumia dawa hizi wataruhusiwa kushiriki lakini kwa kigezo cha kutoiwakilisha Urusi.
Kamati kuu ya Wada imefanya maamuzi haya katika mkutano wake mjini Lausanne, Switzerland.
Hatua hii inakuja baada ya wakala wa kupambana na dawa za kusisimua misuli nchini Urusi (Rusada) kutajwa kutotii na kuziharibu sampuli za wanamichezo wa Urusi Januari 2019.
Hata hivyo ilitakiwa kusiwasilisha sampuli hizo kwa Wada baada ya tuhuma zilizopelekea kufungiwa kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2018.
Wada inasema Rusada ina siku 21 kukata rufaa. Kama haitofanya hivyo pendekezo hilo litafikishwa katika mahakama kuu ya michezo (Cas).
Makamu Rais wa Wada Linda Helleland amesema zuio hili ''halitoshi''
''Binafsi nilitaka kuwepo vikwazo ambavyo vitakua vikali zaidi,'' alisema.''Tunapaswa kuwasafisha wanamichezo ambao hawahusiki na vikwazo hivi kwa kadri tuwezavyo''


EmoticonEmoticon