Dau Waliloliweka Aston Villa Kumpata Mbwanna Samatta, Ripoti Za Usajili

Mbwanna Samatta
Taarifa kutoka katika vyombo vya habari nchini Uingereza leo Januari 16 2020, zinasema kuwa mshambuliaji wa Taifa Stars na klabu ya KRC Genk, Mbwana Samatta yupo mbioni kusajiliwa na klabu ya Aston Villa kwa kwa dau la £10m, inayoshika nafasi ya 18 katika msimamo wa Ligi Kuu Uingereza (EPL).

Kwa mujibu wa ripoti kutoka katika magazeti ya Daily Star  na Mirror zinasema kuwa, Aston Villa inakaribia kukamilisha usajili wa Samatta kwa kiasi cha Pauni milioni 8.5, ambapo hii leo amefanya mazoezi na timu yake lakini anatarajiwa kusafiri hadi nchini Uingereza kukamilisha dili hilo.

Samatta (27) aliifunga bao moja  Liverpool kwenye michuano ya Klabu Bingwa Ulaya (Champions League) na mpaka sasa amefunga mabao 76 katika mechi 191 alizoichezea Genk huku akiwa na mabao 20 katika mechi alizoichezea taifa Stars.

Samatta ambaye alikuwa akihusishwa kutua Crystal Palace yupo katika msimu wake wa nne katika klabu yake Genk, amekataa ofa mbalimbali kutoka klabu za Mashariki ya Kati akishinikiza uhamisho wa kwenda ligi kuu nchini Uingereza ambako ndio ndoto yake ilipo.

Bosi wa Aston Villa, Dean Smith amethibitisha kuwa klabu inahitaji kuongeza nguvu ya kikosi baada ya changamoto walizopata katika mzunguko wa kwanza, “tunalifanyia kazi hilo muda wote, ninafikiri tutakamilisha kabla ya Jumapili”, alisema.

Aston Villa haipo katika nafasi nzuri katika msimamo wa EPL,  kwa sasa  inahitaji mshambuliaji wa kati, kuziba nafasi ya mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Wesley ambaye amepata majeraha.


EmoticonEmoticon