Mshukiwa Wa Virusi Vya Corona Apelekwa Hospital Haraka Kenya

Taarifa zinaeleza kuwa mtu mmoja anayeshukiwa kuwa na virusi vya Corona nchini Kenya amepelekwa hospitalini.
Mshukiwa huyo ambaye ni mwanafunzi amefikishwa hospitali kuu ya rufaa ya Kenyatta jijini Nairobi.
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa mtu huyo aliwekwa karantini alipowasili katika uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Nairobi, msafiri huyo raia wa Kenya alikua akitokea katika jiji la Guangzhou China na aliruhusiwa na maafisa afya wa Uchina kusafiri.
Hata hivyo, baada ya kuwasili jijini Nairobi maafisa afya katika uwanja wa Kenyatta walimuweka katika uangalizi maalumu kabla ya kuhamishiwa hospitali.
Hapo jana Kenya iliitahadharisha raia wake kwenda mji wa Wuhan China, mpaka pale mlipuko wa virusi hivyo utakapodhibitiwa.
Wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ilisema ilikuwa na mawasiliano na raia wake waliokwama katika mji wa Wuhan, mji ambao ni kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo, ambao uko kwenye uangalizi maalum.
''Ubalozi unafahamu kuwa kuna raia wa Kenya 85 mjini Wuhan ambao wamesajiliwa ubalozini hivyo unafuatilia kwa karibu hali hiyo,'' wizara ilieleza kwenye taarifa yake hapo jana.
Kwenye mtandao wa Twitter , wakitoa ujumbe wao wa #KenyansInWuhan, wakenya waliokwama mjini Wuhan walitoa wito kwa serikali yao iwaondoe kwenye mji huo.
''Ni masikitiko tu kwa nchi yetu. Wiki ya pili sasa kwenye mji huu na hakuna lolote linalofanyika,'' aliandika kwenye ukurasa wa Twitter Cornelius Mulili.
''Hali hapa ni mbaya. Ilichofanya serikali yetu ni kutia taarifa kwa vyombo vya habari pekee. Sitaki kueleza tunachokipitia hapa kimwili na kiakili,'' alieleza Rono Kipkorir.
Tahadhari ya kusafiri imekuja siku chache baada ya maafisa nchini Ivory Coast kubaini mgonjwa aliyekuwa na dalili zinazofanan na mtu mwenye virusi vya corona. Haijathibitishwa kama mgonjwa huyo ana virusi hivyo.
Kenya ina moja kati ya viwanja vilivyo na pilikapilika nyingi barani Afrika na imeongeza umakini katika uangalizi wake. Inawapima abiria wote kutoka China.
Credit:Bbc


EmoticonEmoticon