Dogo Wa Miaka 19 Ambaye Messi Na Ronaldo Hawamwambii Lolote Kwenye Rekodi Yake Na Umri Mdogo

Magoli 39. Magoli 11 katika mechi saba za Borussia Dortmund. Magoli 10 katika mechi saba za Klabu Bingwa Ulaya. Yote hayo akiwa na umri wa miaka 19 tu.
Takwimu za ufungaji wa Erling Braut Haaland kwa msimu huu ni ngumu kuziamini.
Bila kusahau amefunga magoli matatu kwenye mechi moja (hat-trick) katika michezo sita.
Usiku wa jana Jumanne, Haaland aliendeleza kasi yake kwa kupachika magoli mawili wakati timu yake ya Dortmund ikiifunga PSG 2-1 kwenye raundi ya kwanza ya mtoano wa Klabu Bingwa Ulaya.
Haaland jana usiku ameweka rekodi ya kufikisha magoli 10 ya Klabu Bingwa Ulaya kwa haraka zaidi, baada ya kucheza mechi saba, rekodi iliyopita ilikuwa magoli 10 katika mechi 11.
Pia amekuwa mchezaji wa kwanza wa umri wa chini ya miaka 20 kufikisha magoli 10 katika Klabu Bingwa Ulaya katika msimu mmoja.
Kylian Mbappe, hakuliweza hilo na hata washambuliaji hatari wa zama hizi Cristiano Ronaldo na Lionel Messi hawakupata rekodi hizo wakiwa na umri wake.
Kwa taarifa yako tu, msimu huu wa 2019-20 Haaland ana magoli mengi zaidi kuliko kikosi chote cha Barcelona katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.
Haaland pia amekuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Dortmund kufunga katika mechi yake ya kwanza ya ligi ya Bundesliga, mechi ya kwanza ya Kombe la Ujerumani na mechi ya kwanza ya Klabu Bingwa Ulaya.
Na kwa sasa kinda huyo ni kinara wa magoli katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa sawa na mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski.

Lakini pamoja na yote hayo, Haaland wala si mtu wa majivuno.
"Nafurahi kupata tuzo ya mchezaji bora, lakini naamini naweza kufanya zaidi ya hapa," amesema baada ya mechi ya jana usiku na kuongeza: "Inanipasa nicheze vizuri zaidi kwenye kiwango hiki, niongeze bidii zaidi."

"Matokeo haya bado ni ya hatari kwetu, PSG wana kikosi kikali na wanaweza wakapita katika raundi ya pili. "


EmoticonEmoticon