Jeshi La Israeli Lafanya Shambulio Kubwa, Ripoti Za Vifo Na Majeruhi Zatangazwa

Jeshi la Israeli linasema limefanya mashambulio ya anga dhidi ya kundi la wanamgambo wa Kipalestina mjini Gaza na Syria kujibu mashambulio yake ya roketi.
Jeshi la Israeli linasema limeyapiga maeneo ya Jihad kusini mwa mji mkuu wa Syria Damascus na katika ukanda wa Gaza siku ya Jumapili.
Katika hatua ya nadra ya Israeli kukubali mashambulio dhidi ya Syria, jeshi la Israeli lilisema kuwa lililenga " kitovu cha shughuli za kundi la jihadi la Kiislamu ".
Syria imesema kuwa majeshi yake ya ulinzi ya anga yalidungua makombora mengi ya Israeli.
Watu wanee walijeruhiwa mjini Gaza, kulingana na maafisa wa afya, lakini hakuna ripoti za moja kwa moja juu ya vifo kutokana na mashambulio ya Israeli.
Mashambulio yalifanywa baada ya eno la kusini mwa Israeli kupigwa na kundi la makombora takriban 20 ya roketi yaliyorushwa mapema jumapili. Hakuna ripoti juu ya majeruhi kwa upande wa Israeli
Uhasama huu ulianza Jumapili , wakati Israeli iliposema ilimuua mjumbe wa kikundi cha Jihad kwenye maeneo ya uzio wa mpaka na ukanda wa Gaza.
Jeshi la Israeli limesema kuwa mwanaume huyo alikua akijaribu kuweka mtambo wa vilipuzi.
Mkanda wa video uliosambazwa sana kwenye mitandao ya habari ya kijamii ilionyesha tingatinga la Israeli likiuburuza mwili wa mwanaume huyo, jambo lililoibua ghadhabu miongoni mwa Wapalestina.
Baadhi ya Wapalestina walitoa wito wa ulipizaji kisasi na saa kadhaa baadae, maroketi yakafyatuliwa katika ukanda wa Gaza na ndipo uvamizi wa anga ukaanza.
Kundi la Jihad la kiislamu lilidai kuhusika na shambulio la maroketi, likiyataja kuwa ni jibu la mauaji ya mmoja wa wapiganaji wake aliyeuliwa kwenye eneo la mpaka wa Gaza.
Kundi la Kiislamu la Jihad, ambalo linaungwa mkono na Iran, ni mojawapo ya makundi yaliyo imara zaidi ya wanamgambo katika Gaza. Likiwa ni mshirik mkuu wa Hamas, limekuwa likipigana vita kadhaa dhidiya Israeli katika miongo ya hivi karibuni.


EmoticonEmoticon