Marufuku Yawekwa Ya Mahusiano Baina Ya Wanafunzi Na Wafanyakazi

Marufuku ya kuwa na uhusiano wa mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha London ni mwamko mpya kwa vyuo vikuu, wachambuzi wamesema.
Makundi ya wanafunzi yamesema kwamba ni imani yao kuwa sera sawia na hiyo zitaanza kutekelezwa na vyuo vingine.
Chuo Kikuu cha London kinaaminika kuwa cha tatu nchini Uingereza kuanzisha marufuku hiyo.
Inasemekana kwamba sera hiyo inalenga kuzuia unyanyasaji kwa walio na madaraka na vitendo vya ngono.
Kelsey Paske, maneja wa kitengo kinachoangazia tabia ya utamaduni, amesema sera hiyo pia inalenga kutatua migogoro ambayo huenda ikazuka kutokana na mahusiano "huenda yakawa na athari mbaya katika mazingira ya kwenye taasisi za masomo".
Sera mpya ya mahusiano katika Chuo Kikuu cha London kwa wafanyakazi, kulingana na gazeti la the Guardian, inakataa "mahusiano ya karibu na ya mapenzi kati ya wafanyakazi na wanafunzi pale ambapo kuna usimamizi wa moja kwa moja".
Uhusiano wa mapenzi kati ya mfanyakazi na mwanafunzi ambaye hamsimamii kimasomo moja kwa moja ni lazima uwekwe wazi na mfanyakazi.
Sera hiyo pia inakataza mahusiano ya mapenzi na wafanyakazi au wanafunzi wenye umri wa chini ya miaka 18 au watu wazima ambao wako katika hatari mfano, yule ambaye atahitaji usaidizi maalumu kwasababu nya ulemavu.
Kukiuka sera hiyo kutachunguzwa na kitengo cha kukabiliana na utovu wa nidhamu chuoni, ambao ni pamoja na uwezekano wa kuchukuliwa kwa hatua kuanzia kupewa onyo rasmi hadi kufutwa kazi au kufukuzwa chuoni.


EmoticonEmoticon