Raisi Donald Trump Awafuta Kazi Viongozi 2 Waliomshuhudia, Viongozi Hao Wazungumza Haya

Rais Donald Trump amewafuta kazi maafisa wawili waandamizi waliotoa ushahidi dhidi yake katika kesi ya kutokuwa na imani naye iliyokuwa inamkabili.
Balozi wa Marekani kwa Muungano wa Ulaya, Gordon Sondland, amesema "Nimeambiwa kwamba rais anataka nirudi nyumbani mara moja".
Awali, Luteni kanali Alexander Vindman, mtaalamu mkuu katika masuala ya Ukraine, alisindikizwa kutoka nje ya Ikulu ya Marekani.
Inasemekana kwamba Bwana Trump amesema anataka kufanya mabadiliko baada ya bunge la Seneti kumuondolea mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Jumatano.
Katika kura ya kihistoria iliyopigwa, Bunge la Seneti limeamua kutomuondoa rais huyo wa 45 wa Marekani madarakani kwa madai yaliyokuwa yameibuliwa dhidi yake kutokana na mahusiano yake na Ukraine.
Kaka yake Luteni kanali Vindman ambaye pia ni pacha mwenzake, Yevgeny Vindman, wakili mwandamizi katika baraza la Usalama la taifa pia alirejeshwa katika idara ya jeshi Ijumaa.
Katika taarifa iliyotolewa na wakili wake, bwana Sondland amesema: "Nimearifiwa hii leo kwamba rais anataka nirudi nyumbani mara moja baada ya kunivua wadhifa wa balozi wa Marekani kwa Muungano wa Ulaya.
"Nashukuru kwa fursa ambayo Rais Trump alinipa ya kuhudumia taifa, pia namshukuru Waziri wa mambo ya nje Mike Pompeo kwa kuniunga mkono, na tena shukrani zangu ziwaendee wafanyakazi wote wa ubalozini wa Muungano wa Ulaya kwa utalaamu wao na kujitolea kwao.
Gordon Sondland
"Najivunia kile ambacho tumefikia. Kazi yetu hapa imekuwa kielelezo chema kwa taaluma yangu," Bwana Sondland amesema.
Mshauri wa Luteni kanali Vindman, David Pressman, ameiambia BBC kwamba mteja wake ametolewa nje ya Ikulu ambako amekuwa akifanya kazi yake kwa uadilifu kwa nchi yake na kwa rais wake".
Alexander Vindman
"Hakuna raia yeyote wa Marekani anayejiuliza kwanini raia huyu amefutwa kazi, kwanini nchi hii sasa ina mtu mmoja tu mwenye nguvu anayeongoza Ikulu ya Marekani," taarifa hiyo imesema.
"Luteni Vindman alifutwa kazi baada ya kusema ukweli Heshima yake, kujitolea kwake kufanya kilicho sawa, kulitia hofu wenye nguvu."
Taarifa hiyo imeongeza: " Ukweli umemgharimu Alexander Vindman kazi yake, taaluma yake, na faragha yake."
Luteni kanali Vindman alifika kazini Ijumaa katika Ikulu kama kawaida.
Credit:Bbc


EmoticonEmoticon