Baada Ya Kukimbia Corona Cristiano Ronaldo Na Familia Yake, Mazito Mengine Yawakumba Walikokimbilia

Straika wa Juventus, Cristiano Ronaldo amekimbia mlipuko wa virusi vya corona nchini Italia, lakini bahati mbaya kwake amekutana na tetemeko la ardhi nyumbani kwao Madeira, Ureno.

Matetemeko mawili yalipita katika mji wa Funchal katika visiwa hivyo ambako Ronaldo amejificha na familia yake mara baada ya kuondoka Italia mapema wiki iliyopita.

Baada ya mama yake, Dolores kupata tatizo la kupooza staa huyo wa Juventus alirudi kwao Madeira kwa ajili ya kukaa na familia yake, kabla ya kupata taarifa za kusimamishwa kwa Ligi Kuu Italia na kuamua kubaki nyumbani kwao. Lakini, juzi kati alishuhudia mji huo ukipigwa na matetemeko mawili makubwa.

Kwa mujibu wa taarifa, tetemeko la kwanza lilikuwa na kipimo cha Richter 3.8, kabla ya kufuatiwa na tetemeko kubwa zaidi la 5.2. Hakuna mtu aliyeumia kwenye matetemeko hayo, japokuwa kumekuwa na taarifa kuwa mawe makubwa na miti yameziba barabara za kisiwa hicho baada ya tetemeko.

Madeira ni sehemu ambayo imekuwa ikikutwa na matetemeko ya mara kwa mara, ambapo tetemeko la karibuni lilitokea kilomita 10 kutoka kwenye visiwa hivyo.


EmoticonEmoticon