Corona Yaendelea Kusambaa Kwa Kasi Kenya, Visa Vipya Vyatangazwa

Watu tisa zaidi wamekutwa na virusi vya ugonjwa wa corona, na hivyo basi kuweka jumla ya watu waliopatikana na ugonjwa huo Kenya kufikia 59.
Wakati wa mkutano na wanahabari, katibu wa huduma za Afya nchini humo Mercy Mwangangi amesema kwamba sampuli 234 zilifanyiwa vipimo na watu tisa wakakutwa na virusi hivyo.
Bi Mwangangi amesema kwamba maafisa kwa sasa wanawasaka watu ambao huenda walikaribiana na wagonjwa hao.
Mwangangi amesema kwamba serikali inachunguza watu wengine 1,160.
''Endeleeni kukaa mbali mbali na mutumie nambari ya bila malipo,'' ametoa rai.
Serikali tayari imewataka wale wanaoishi Nairobi kutoelekea katika maeneo ya mashambani wakati huu kwa kuwa idadi kubwa ya wazee wanaishi katika maeneo hayo.
Wenye makampuni pia wametakiwa kuwaachilia wafanyakazi wao mwendo wa saa kumi, ili kuwaruhusu kwenda nyumbani kabla ya amri ya kutotoka nje kuanza kutekelezwa kuanzia mwendo wa saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri.
Kutokana na habari iliotolewa na serikali tangu kisa cha kwanza mnamo tarehe 13 mwezi Machi, kuna raia 10 wa kigeni ambao ni miongoni mwa wagonjwa 59 waliokutwa na virusi hivyo.
Kati ya kumi hao ni raia wawili wa Ufaransa, ambao mmoja wao yuko katika chumba mahututi katika hospitali ya Agha Khan.
Wawili wengine ni raia wa DR Congo, mmoja raia wa Mexico mmoja raia wa China na mmoja raia wa Burundi. Wengine ni raia mmoja wa Marekani, raia wa Cameroon na mmoja wa Burkina fasso.EmoticonEmoticon