Messi Akana Stori Za Kumlipia Ronaldinho Dhamana, Waendelea Kusota Rumande


Ronaldinho na kaka yake Roberto wanaendelea kusota rumande kwa tuhuma za kuingia Paraguay kwa kutumia hati za kusafiria za kugushi na maombi yao ya dhamana yameendelea kutupwa na mahakama.

Hivi karibuni wawili hao walituma maombi ya dhamana yenye thamani ya Pauni 1.26 milioni ili watoke sero na kukaa nje wakati wakisubiri kujua hatma yao, lakini maombi hayo yalikataliwa na Jaji Gustavo Amarilla.

Maombi ya dhamana ya Ronaldinho na kaka yake yalitumwa kupitia Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali, lakini Jaji Amarilla aliyakataa kwa madai kuwa wawili hao wanaweza kutoroka.

Inaelezwa kuwa mamlaka za kisheria za Paraguay zinaamini kuwa pesa ambayo Ronaldinho alitaka kutoa kwa ajili ya dhamana yake ni ndogo sana kulinganisha na uwezo halisi wa kifedha wa staa huyo.

Katika maombi hayo wakili wa Ronaldinho anadaiwa kuionyesha mahakama jumba la thamani ya Euro 800,000 ambalo litatumika kama kizuizi kwa Gaucho na kaka yake wakiwa nje, lakini hilo halikutosha kuishawishi mahakama kutoa dhamana.

Ronaldhinho na kama yake wamesota rumande tangu Machi 6, mwaka huu, walipoingizwa kwa mara ya kwanza baada ya hakimu kutoa amri ya kukamatwa kwao.

Wakati hayo yakiendelea straika wa Barcelona, Lionel Messi amekanusha taarifa kuwa alitaka kutoa kiasi cha Pauni 3.25 milioni ili kufanikisha kuachiwa huru kwa staa huyo ambaye waliwahi kucheza pamoja Nou Camp.

Awali kulikuwa na taarifa kuwa Messi alipanga kuajiri wanasheria bora wanne kwa ajili ya kusimamia kesi ya Ronaldinho, huku akidaiwa kutenga jumla ya Pauni 3.25 milioni kufanikisha hilo.

Hata hivyo, taarifa hizo zimepingwa na watu wa Messi ambao wamedai kuwa licha ya kwamba staa huyo anamuonea huruma Ronaldinho, lakini taarifa za kwamba atatumia pesa zake kumtoa rumande ni uzushi mtupu.


EmoticonEmoticon