Serikali Ya Kenya Yatoa Masharti Makali Kwenye Kumbi Za Burudani, Daladala Na Wafanyakazi Wa Maofisini

Licha ya kwamba hakuna kisa kipya cha virusi vya Corona, lakini serikali ya Kenya imetangaza makatazo mengine kwa umma.
Kuanzia sasa maduka makubwa yameagizwa kudhibiti idadi ya wateja, kipaumbele kikipewa wanawake wajawazito, wazee na walemavu.
Maeneo ya burudani kufungwa ifikapo saa moja unusu usiku kuanzia Jumatatu ijayo kama jitihada za kudhibiti virusi vya Corona.
Awali maeneo ya burudani yaliruhusiwa kuhudumu hadi saa tano usiku.
Daladala zinazobeba watu 14 kwa kawaida sasa zimeagizwa kubeba abiria wanane pekee, yanayobeba watu thelathini kubeba asilimia sitini pekee ya abiria.
Agizo hilo pia linatumika katika usafiri wa treni.
Maafisa wa afya wataanza kunyunyiza dawa za kuua viini katika maeneo ya umma wakianzia soko kubwa la Gikomba, siku ya Jumamosi ambayo pia ni siku ya maombi ya kitaifa.
Waajiri wameagizwa kuhakikisha wafanyakazi wao hawakaribiani na kampuni zitachukuliwa hatua iwapo hawatazingatia hayo na waajiriwa wao watakumbwa na Corona.
Kenya imechukua hatua kadha wa kadha kujaribu kupambana na virusi hivyo ikiwemo kufunga shule na vyuo vikuu kote nchini, kupunguza safari za ndege na kupiga marufuku mikutano ya hadhara na mikusanyiko ya watu.


EmoticonEmoticon