Chanjo Mbili Za Corona Zaanza Kufanyiwa Majaribio

Wanasayansi nchini Australia wameanza kufanya majaribio ya dawa mbili zinazoweza kuwa chanjo dhidi ya virusi vya corona.
Hiyo inatajwa kuwa ni "hatua muhimu " ya majaribio ya maabara.
Chanjo hizo zilizotengenezwa na Chuo Kikuu cha Oxford na kampuni ya Marekani ya madawa - Inovio Pharmaceutical, zimeidhinishwa kufanyiwa majaribio kwa wanyama na Shrika la Afya Duniani (WHO).
Shirika la taifa la sayansi nchini Australia litatathmini kama chanjo hizo zinafanya kazi, na iwapo zitakuwa salama kwa binadamu.
Majaribio ya kwanza kwa binadamu yalifanyika nchini Marekani mwezi uliopita, lakini hata hivyo yaliruka hatua ya majaribio kwa wanyama.
Kuna chanjo nyingine kadhaa zinazofanyiwa uchunguzi katika maeneo mbali mbali duniani kwa sasa kwa kasi isiyo ya kawaida.
Lakini wanasayansi wa Jumuiya ya Madola wa Australia na Shirika la Utafiti wa kisayansi (CSIRO) wanasema vipimo vyao vitakuwa ni vya kwanza vilivyokamilika vya kutumia mnyama kabla ya kufanyika kwa vipimo halisi vya kliniki.
Watafiti wanasema kasi na kiwango cha ushirikiano uliowawezesha kufikia hatua hii havikutarajiwa.
"Kwa kawaida inaweza kuchukua takriban mwaka mmoja hadi miwili kufikia hapa tulipo, na kusema ukweli tumefupisha kipindi hicho hadi miezi," Dkt Rob Grenfell kutoka CSIRO amewaambia waandishi wa habari Alhamisi.


EmoticonEmoticon