CORONA : Shirika La Afya Duniani Limelaani Kauli Ya Kibaguzi Kuhusu Chanjo Ya Corona Kufanyiwa Majaribio Afrika

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amelaani kauli alizoziita za "kibaguzi" kutoka kwa madaktari wawili wa Ufaransa ambao walitaka chanjo ya virusi vya corona kufanyiwa majaribio barani Afrika.
"Afrika sio na haitakuwa uwanja wa majaribio wa chanjo yoyote," amesema Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus.
Matamshi ya madaktari hao waliyoyatoa kwenye mjadala wa runinga yamezua ghadhabu, na wametuhumiwa kwa kuwachukulia Waafrika kama "nguruwe wa kufanyiwa majaribio ya maabara".
Mmoja wa madaktari hao ameomba radhi kwa kauli yake.
Alipoulizwa kuhusu matamshi ya madaktari hao kwenye mkutano na wanahabari juu ya hali ya virusi vya corona ulimwenguni, Dkt Tedros alionekana Dhahiri kuwa mtu mwenye hasira, na kukiita kitendo cha madaktari hao kama "mning'inio kutoka kwenye ulevi wa fikra za kikoloni".
"Ni fedheha, jambo la kushtusha kusikia katika Karne ya 21 kutoka kwa wanasayansi wakitoa kauli kama zile. Tunalaani hilo kwa nguvu zote, na tunawahakikishia kuwa hilo halitatokea," ameeleza Dkt Tedros.
Kadri ya namba ya watu wenye virusi vya corona inavyopanda barani Afrika, baadhi ya serikali barani humo zinachukua hatua ngumu na kali za kujaribu kupunguza kasi ya maambukizi.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta hapo jana alipiga marufuku safari zote za kutoka na kuingia Nairobi pamoja na miji mingine mikubwa mitatu kwa kipindi cha wiki tatu.


EmoticonEmoticon