CORONA : Trump Alitupia Lawama Shirika La Afya Duniani Likishirikiana Na China

Rais Donald Trump amelishukia shirika la afya duniani WHO na kulilaumu kwa kuegemea upande wa China.Trump amesema asasi hiyo ya kimataifa ilishirikiana na China kuficha ukweli.

Rais wa Marekani Trump ametishia kulikatia fedha shirika la afya Duniani WHO kwa sababu amesema shirika hilo halikutilia maanani kwa namna ilivyopasa hatari ya maambukizi ya virusi vya corona. 

Trump amelilaumu shirika hilo kwa kuegemea zaidi upande wa China. Rais huyo wa Marekani amedai kwamba asasi hiyo ya kimataifa ilishirikiana na China katika miezi kadhaa iliyopita kupuuza hatari ya maambukizi ya virusi vya corona.

Akitoa taarifa juu ya hali ya maambukizi hayo nchini Marekani, Trump alipuuza umuhimu wa taarifa ya mshauri mwandamizi iliyotolewa mapema mwaka huu kutahadharisha juu ya uwezekano wa kulipuka kwa maambukizi hayo. Rais huyo amedai kwamba hakuiona taarifa hiyo.

Badala yake Rais huyo wa Marekani amelishukia shirika la afya duniani WHO na kulitishia kulikatia fedha.Trump amesema asasi hiyo inaegemea sana upande wa China kuhusu mkakati wake wa kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. 

Amedai kwamba Shirika la WHO lilishirikiana na China katika juhudi za nchi hiyo za kupunguza hatari ya mlipuko wa maambukizi hayo.

Rais Trump amesema Shirika hilo limeisifu China ingawa pana sababu ya kuwa na mashaka juu ya idadi rasmi  iliyotolewa na serikali ya China juu ya vifo vilivyotokana na mambukizi ya virusi vya corona.

Trump amesema WHO ilipaswa kujua juu ya hayo.Tangu aingie madarakani Rais Trump amekuwa anayatilia mashaka mashirika ya kimataifa na mara kwa mara amekuwa analibeza shirika  hilo la afya. 

Katika bajeti ya mwezi Februari utawala wa Trump ulipendekeza kupunguza mchango wa fedha wa Marekani kwa shirika la WHO kutoka dola milioni 122.6 hadi dola milioni 59.9

Shirika hilo la kimataifa lililitangaza mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona kuwa hatari kwa afya ya binadamu wote, tarehe 30 mwezi Januari, takriban mwezi  mmoja kabla ya rais wa Marekani kusema kwenye "twitter” kwamba maambukizi ya virusi vya corona yalikuwa yamedhibitiwa nchini Marekani.


EmoticonEmoticon