Maambukizi Mapya Ni Watu 22 Kenya, Idadi Yapanda Kwa Kasi

Watu 22 zaidi wamekutwa na virusi vya ugonjwa wa corona, na hivyobasi kuweka jumla ya watu waliopatikana na ugonjwa huo Kenya kufikia 81.
Akizungumza na vyombo vya habari waziri wa Afya Mutahi Kagwe hatahivyo amesema kwamba kuna habari njema baada ya wagonjwa watatu kuripotiwa kupona.
Mutahi Kagwe amesema kwamba wagonjwa 13 ni wanaume na tisa ni wanawake. Wagonjwa hao wanashirikisha Wakenya 18, raia 2 wa Pakistan na raia 2 wa Cameroon.
''Tumewapima Wakenya 300 kati yao watu 22 wamekutwa na virusi vya coronavirus . Hii ndio idadi kubwa zaidi kuwahi kupata kwa siku'', alisema.
''Hiyo inakwambia umuhimu wa zoezi ambalo tumekuwa tukifanya kwa kuwa hao wangeambukiza watu wengine'', aliongezea Kagwe.
Waziri Kagwe amesema kwamba wagonjwa wawili waliopona ugonjwa huo Brenda na Brian , wamesisitiza kwa Wakenya kwamba iwapo watakuwa na dalili za Covid-19 wanapaswa kwenda kuripoti katika kituo cha afya.
Amesema kwamba virusi hivyo vinasambaa kwa haraka nchini humo. Kuhusu visa vilivyoripotiwa katika saa 24 zilizopita , waziri amesema kwamba Kakamega imeripoti kisa 1, Kiambu visa 2, Kilifi kisa 1, Mombasa visa 7, Muranga kisa 1, Nairobi kisa 1 na Nyamira kisa 1.
Amewaomba Wakenya kufuatia maelezo ya serikali lakini akasema kwamba magari ya kubeba chakula yanaruhusiwa kusafiri kokote nchini. ''Kile tunachozuia ni mikutano ya watu'' .


EmoticonEmoticon