Burundi Wazima Mitandao Ya Kijamii Kwaajili Ya Uchaguzi

Mitandao ya kijamii imezimwa huku wananchi wakiendelea kupiga kura nchini Burundi katika uchaguzi mkuu hii leo.
BBC imethibitisha kuwa mitandao ya Twitter, Whatsapp na Facebook kuwa haipatikani nchini humo.
Serikali ya Burundi hata hivyo haijalizungumzia suala hilo.
Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa toka saa 12 asubuhi na vitafungwa saa 10 alasiri.
Wagombea saba wanawania hii leo kumrithi Pierre Nkurunziza, hata hivyo wagombea wawili ndio wanaopigiwa upatu zaidi, kutoka chama cha upinzani CNL Agathon Rwasa na chama tawala CNDD-FDD Evariste Ndayishimiye.
Raia wa Burundi wanapiga kura ya kumchagua rais, na katika karatasi za kupigia kura, jina la Pierre Nkurunziza halipo.
Siku ya leo inakamilisha utawala wa bwana Nkurunziza ambaye aliingia madarakani katika taifa hilo la Afrika Mashariki miaka 15 iliyopita.
Uchaguzi huo pia unahusisha nafasi za ubunge na madiwani. Matokeo yanatarajiwa kuanzia Mei 25.


EmoticonEmoticon