Hospitali Za Jiji Kubwa La Brazil Kuzidiwa Na Wagonjwa Wa Corona

Meya wa jiji kubwa zaidi nchini Brazili, São Paulo la Sao Paulo amesema kuwa mfumo wa afya unaweza kuporomoka huku kukiwa na ongezeko la mahitaji ya vitanda vya dharura ili kuwahudumia wagonjwa wa corona.
Bruno Covas amesema hospitali za umma za jiji hilo zinaweza kujaa katika kipindi cha wiki mbili zijazo.
Sao Paulo ni moja kati ya miji iliyoathirika zaidi nchini Brazil kukiwa na watu 3,000 waliopoteza maisha mpaka sasa kutokana na corona.
Siku ya Jumamosi, Brazil ilizidi nchi ya Uhispania na Italia na kuwa taifa la nne lenye idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya corona.
Wizara ya afya imeripoti maambukizi mapya 7,938 katika kipindi cha saa 24, jumla ya watu walioambukizwa ikifikia 241,000.
Marekani, Urusi na Uingereza ndizo zilizo na idadi kubwa zaidi ya watu waliopatwa na maambukizi.
Idadi ya waliopoteza maisha katika nchi hiyo ya Amerika ya Kusini katika kipindi cha saa 24 ni watu 485, ikiwa na jumla ya vifo 16,118, takwimu zinazolifanya taifa hilo kushika nafasi ya tano kati ya nchi zenye idadi kubwa ya vifo.
Wataalamu wa afya nchini Brazil wameonya kuwa idadi kamili ya walioambukizwa nchini humo inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko takwimu zilizotolewa na serikali, kutokana na upungufu wa vipimo.
Rais wa Brazil Jair Bolsonaro amekosolewa vikali ndani na nje ya nchi kwa namna anavyoshughulikia janga la corona linaloendelea kushika kasi.
Alipuuza ushauri wa wataalamu wa afya duniani kuhusu kutochangamana siku ya Jumapili alipopiga picha na watu wanaomuunga mkono na watoto katika mji wa Brasilia.


EmoticonEmoticon