Mambo 12 Yatakayokusaidia Kutathmini Ndoa Yako Ni Nzima Au Imekufa

Kuna wengi wanaojipata katika  hali ya  kutisha ya ndoa zao kufa wakiwa bado ndani. Kuna mambo ambayo yanafaa kuendelea katika ndoa yako lakini kila kitu kimesimama. 

Hizi hapa dalili kwamba upo katika ndoa ‘iliyokufa’ na unafaa kuanza kuchukua hatua za kuifufua au kuamua kufunga virago na kuondoka.

  1. Hakuna tendo la ndoa
Endapo kuna sababu za kimatibabu kutoshiriki tendo la ndoa na mwenzako, basi itaeleweka lakini iwapo kila kitu kipo sawa lakini nyote au mmoja wenu hana hamu na mwenzake basi dalili hii ni mbaya kwa maisha ya ndoa yenu.

2. Huna cha kumuambia mwenzake
Iwapo kuna jambo linalokufanyikia kazini au umesajili mafanikio fulani na mwenzako sio miongoni mwa watu wa kwanza kujuzwa, basi kwisha mambo. Humuoni kama mtu muhimu katika maisha yako anayefaa kufahamu yote yanayofanyika katika maisha yako. Endapo utapata ugumu wa kufanya gumzo za hapa na pale na mwenzako katika ndoa, basi umefika mwisho na umechoka.

3. Mko pamoja lakini sio  pamoja
Endapo mtajipata katika nyumba moja na kila mtu anajishughulisha na mambo yake bila utangamano wa pamoja basi mko pamoja kwa njia tofauti. Hatua hiyo humaanisha kwamba hakuna tena kinachowaunganisha kwa dhamira moja.

 4.Unajishughulisha na mambo na matatizo ya watu wengine
Wanawake wana mazoea ya kujishughulisha na matatizo ya watu wengine ili kuficha machungu wanayopitia. Endapo utajipata unajiingiza sana katika masuala ya wengine basi dalili hiyo ni ya kwamba unajaribu kujishughulisha ujipe muda mbali na masaibu yako.

5. Pengo kati yenu linazidi kupanuka
Endapo utajipata kwamba kila wakati mnapozungumza malumbano yanazuka na kuwatenganisha  zaidi, basi dalili hiyo sio nzuri. Ni kawaida kwa wanandoa kupitia nyakati ngumu lakini zikianza kudumu kwa muda mrefu basi zitakuwa mtindo wa kila siku na kuvuruga ndoa yenu.

6. Unaanza kutamani maisha bila mwenzako
Iwapo utawahi kufikiria kuhusu uwezo wako kuwa na furaha bila mwenzako maishani mwako, basi hilo sio jambo zuri. Hiyo ni mojawapo ya hatua za kujiondoa kihisia kutoka kwake na ni dalili kwamba mambo kati yeni yamevurugika kwa kiwango kikubwa.

 7. Mmeacha kupigana
Endapo mtakoma kupigana au malumbano kwa kusalimu amri, ni ishara kwamba mmefika mwisho wa safari yenu ya ndoa. Anachofanya mwenzako hakikwazi na hivyo basi hujali kuhusu maamuzi au mkondo anaochukua.

 8. Unahisi kwamba hakusikizi
Endapo mmoja wenu atahisi kana kwamba mwenzake hampi muda wa kumsikiza au kuzingatia mchango wake katika ndoa basi dalili hiyo ni mbaya kwa ndoa yenu. Njia bora ya kusuluhisha mizozo katika ndoa sio tu kuelewa tatizo bali pia kusikiliza kuanzia mwanzo.

 9. Unawatembelea  marafiki zako badala ya mwenzako
Unapojipata unatafita sababu za kuwatembelea rafiki zako badala ya mume au mkeo basi fahamu kwamba mambo yamevuka mipaka. Endapo kumuona mwenzako kunazua makovu na hamaki ya matatizo ambayo hamkuyasuluhisha ni daalili kwamba mnafaa kuanza kutafuta njia za kujikwamua kutoka hali hiyo.

10. Hamna muda pamoja
Unapofika nyumbani baada ya siku ndefu ya kazi na uchovu, mnakaa pamoja sebuleni au kila mtu anaendelea na shughuli zake? Endapo hakuna aliye na muda na mwenzake, dalili hiyo sio nzuri kwa ndoa yenu.

 11. Hayupo katika orodha ya vipaumbele
Wapendanao hujali sana kuhusu wenzao katika ndoa na iwapo utajipata huna muda hata wa kumfikiria au kujali kuhusu anachofanya, basi fahamu kwamba kuna tatizo na ndoa yenu ipo katika hatua mbaya.

12.  Mwenzao hayuko tayari kufanya juhudi za kuboresha ndoa yenu
Endapo umejipata katika kibarua cha kuikwamua ndoa yenu peke yako na mwenzio hana mbio, basi jua kwamba ndoa hiyo imefika tamati.


EmoticonEmoticon