Marekani Kukabiliwa Na Kipindi Kibaya Zaidi Cha Corona

Afisa wa zamani wa ngazi ya juu wa afya nchini Marekani ameliambia bunge la kongresi kuwa nchi inaweza kukabiliwa na "kipindi kibaya zaidi cha majira ya baridi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya hivi karibuni " kwa sababu ya virusi vya corona.
Rick Bright aliongoza shirika la serikali kujaribu kutengeneza chanjo,lakini akaondolewa katika kazi hiyo mwezi uliopita.
Awali alisema aliondolewa kazini kwa kuelezea hofu juu ya tiba zinazotangazwa na rais Donal Trump.
Rais Trump alimfuta kazi kwa madai kuwa alikua mtumishi "asiyeridhika"
Bwana Bright pia aliiambia kamati ya Bunge la wawakilishi ya masuala ya afya kuwa ''maisha yanapotea'' kwa sababu ya serikali "kutochukua hatua " katika hatua za mwanzo za mlipuko wa virusi vya corona.
Alisema kuwa kwa mara ya kwanza alizungumzia juu ya ukosefu wa zana za matibabu mwezi Januari, na kufikisha suala hilo katika "ngazi za juu" za Wizara ya Afya na huduma za binadamu (HHS), lakini "hakujibiwa".

Wakati wa ushahidi, Bwana Bright alionya kwamba " dirisha " la kushughulikia virusi vya corona linakaribia "kufunga".
"Kama tutashindwa kuboresha jinsi tunavyokabiliana na ugonjwa huu sasa, kwa misingi ya sayansi, ninaogopajanga litakua baya sana na kuendelea kwa muda mrefu ," alisema.
"Bila mpango bora, 2020 unaweza kuwa na kipindi kibaya zaidi cha majira ya baridi kuwahi kushuhudiwa katika histioria ya sasa ."
Bwana Bright pia ameiambia kamati hiyo ya bunge la wawakilishi kuwa mwezi Januari alipokea barua pepe ambayo "hawezi kusahau ", kutoka kwa wasambazaji wa barakoa za hospitali ambao walioonya juu ya upungufu mkubwa wa barakoa,
"Alisema... tunahitaji kuchukua hatua.Na nikaituma barua hiyo kwa ngazi ya juu ya HHS - na sikupata jibu."
Bwana Bright alisema kuwa kuondolewa kwake kazini kulikua ni matokeo ya kuendelea kwake kusisitiza kwamba pesa zilizotengwa na Kongresi za kukpambana na mlipuko wa virusi zinapaswa kuwekwa "katika suluhu salama na zilizochunguzwa kisayansi na sio katika madawa , chanjo au teknolojia nyingine ambazo hazijathibitishwa kisayansi ".
"Nilizungumza wazi wakati ule, na ninatoa ushahidi leo, kwa sababu sayansi sio siasa au upendeleo -lazima iongoze katika njia ya kupambana na virusi," aliongeza.


EmoticonEmoticon