Namna Majasusi Wanavyohangaika Na Mtandao Kuiba Siri Za Chanjo Ya Corona

Majasusi nchini Marekani wanaripoti kuona taasisi za kijasusi za nchi nyengine wakijaribu kupitia mtandao kuchunguza tafiti za chanjo ya virusi vya corona nchini humo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Ulinzi na Kukabiliana na Ujasusi wa Kimataifa cha Marekani Bill Evanina, ameiambia BBC kuwa serikali ya nchi hiyo tayari imeshatoa onyo kwa vituo vya utafiti wa kitabibu juu ya hatari ya kijasusi iliyopo.
Hata hivyo hakubainisha kama kumetokea wizi wowote wa taarifa kuhusu maendeleo ya tafiti za chanjo.
Vyanzo vetu vya usalama nchini Uingereza pia vimetuambia kuwa vimeona majaribio hayo ya kijasusi yakitokea.
Mashindano ya kutafuta chanjo
Kwa sasa kuna mbio za kimataifa zinazoendelea katika kutafuta kinga ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.
Watafiti, makampuni binafsi na serikali mbali mbali zinashiriki katika kutafuta chanjo. Na juhudi zao zinalindwa na taasisi za kijasusi za mataifa hayo, huku zikiwa zinalengwa na mashirika ya kijasusi ya nchi nyengine.
Kituo kinachoongozwa na Bwana Evanina kinatoa ushauri kwa serikali ya Marekani, makampuni na wasomi juu ya namna ya kujilinda na mashambulizi kutoka katika taasisi za kijasusi za nchi nyengine.
"Tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na watu kutoka serikalini na makampuni ili kuhakikisha tafiti zote na taarifa zake zinalindwa vilivyo," amesema.
"Tunatarajia kuwa taasisi za kijasusi za kigeni, pamoja na Chama Cha Kikomunisti cha Uchina, watajaribu kupata kile tukifanyacho hapa."
Serikali ya Marekani inajaribu kusaidia shughuli za utafiti kwa kuandaa operesheni maalumu.
Nchi yoyote ambayo itakuwa ya kwanza kupata chanjo salama na inayofanya kazi kwa ufanisi itawawezesha wananchi wake awali kufaidika na kuwa salama.
"Tumekuwa tukiwasiliana na kila taasisi ya utafiti wa matibabu ili wachukue hatua zaidi za kujilinda," ameeleza Bw Evanina.
"Katika dunia ya leo hakuna kitu cha muhimu kuiba kama taarifa za kitafiti ambazo zitakusaidia kupata kinga dhidi ya virusi vya corona."
Credit:Bbc


EmoticonEmoticon