Polisi Waliosababisha Kifo Cha Mtu Mweusi Wachukuliwa Hatua Kali (VIDEO)

Maafisa wanne wa polisi katika jimbo la Minnesota nchini Marekani wamefutwa kazi kufuatia kifo cha mtu mweusi ambaye alikuwa amekamatwa na kuonekana akizuiliwa chini kwa kushikwa shingo.
Afisa mkuu wa polisi katika jimbo hilo Medaria Arradondo amesema kwamba maafisa hao wanne sasa ''sio wafanyakzi wa kikosi hicho''.
Kanda ya video inaonesha, mtu huyo kwa jina George Floyd , akilia na kuwaambia maafisa hao weupe ''siwezi kupumua''.
Kisa hicho kinafanana na kile cha Eric Garner, mtu mweusi aliyefariki akikamatwa na polisi mjini New York mwaka 2014.
Shirika la ujasusi nchini Marekani FBi lilisema litachunguza kisa hicho cha Minneapolis kilichofanyika Jumatatu jioni.
Maafisa wa polisi wa Minnesota walisema kwamba Floyd mwenye umri wa miaka 46 , ambaye alikuwa anafanya kazi kama afisa wa usalama katika mkahawa mmoja alifariki akifanyiwa matibabu kufuatia malumbano na maafisa wa polisi.
Siku ya Jumanne, Meya Jacob Frey alithibitisha kwamba maafisa hao wanne waliohusishwa na kisa hicho wamefutwa kazi. ''Huu ndio uamuzi tuliochukua''.
Katika mkutano na vyombo vya habari mapema, bwana Frey alikitaja kisa hicho kama cha kushangaza.
''Ninaamini kwamba kile nilichokiona ni kitendo cha makosa kwa kiwango chochote kile'' , alisema.
''Kuwa mtu mweusi nchini Marekani hakustahili kuwa hukumu ya kifo''.


EmoticonEmoticon